2014-04-04 15:03:12

Salam na matashi mema kwa Patriaki Ignatius Aphrem II


Baba Mtakatifu Francisko amemwandikia ujumbe wa matashi mema Patriaki Ignatius Aphrem II, aliyechaguliwa hivi karibuni kuongoza Kanisa la Kiorthodox la Antiokia na Syria. Baba Mtakatifu anachukua fursa hii kumtakia kheri, baraka tele pamoja na mshikamano wa kidugu Patriaki pamoja na waamini wake, kwa kumwombea baraka kutoka kwa Roho Mtakatifu ili aweze kutekeleza dhamana na utume wake kwa Kanisa.

Ni matumaini ya Papa Francisko kwamba, Patriaki mpya atakuwa kweli ni Baba wa maisha ya kiroho, kwa kujenga na kuimarisha umoja, mshikamano na amani kati ya wananchi wanaoishi Mashariki ya Kati, licha ya hali ngumu wanayokabiliana yao. Wakristo wanaalikwa kutolea ushuhuda wa imani yao kwa Kristo na Kanisa lake, kwa kukazia mambo msingi yanayowaunganisha Wakristo, kama inavyojionesha katika ile sala ya Kikuhani iliyotolewa na Yesu mwenyewe, ili wote wawe wamoja ili ulimwengu uweze kuamini.

Mwishoni, Baba Mtakatifu anapongeza ushirikiano uliopo kati ya Kanisa la Kiorthodox la Syria pamoja na Kanisa Katoliki na ni matumaini yake kwamba, uhusiano huu utaendelea kuimarika na kuboreka zaidi.







All the contents on this site are copyrighted ©.