2014-04-04 10:20:11

Majandokasisi 11 kupewa daraja la ushemasi mjini Roma!


Askofu Anders Arbolieus wa Jimbo Katoliki la Stockholm, Sweden, Jumamosi tarehe 5 Aprili 2014 anatarajia kutoa Daraja Takatifu la Ushemasi kwa Mafrateri kumi na moja kutoka Shirika la Bikira Maria wa Mlima Karmel. Mafrateri wafuatao ni kutoka Barani Afrika. Frt. Charles Adeniyi, Nigeria; Frt. Christian Chinedu Odo, Nigeria; Frt. Razafimahatratra Richard kutoka Madagascar pamoja na Frt. Elius Modest Malale kutoka Jimbo Kuu la Tabora, Tanzania anayetusimulia kwa ufupi historia ya wito wake wa maisha ya kitawa. RealAudioMP3

Mimi Frt. Elius Modest Malale wa Shirika la Bikira Maria wa Mlima Karmeli nimezaliwa tarehe 10/12/1977 katika kijiji cha Uyogo, Wilaya ya Urambo, Mkoa wa Tabora, nchini tanzania. Nilisoma shule ya msingi Uyogo na kuhitimu elimu ya shule ya msingi mwaka 1993. Sikuweza kuendelea na masomo ya sekondari kwa wakati huo, kwa kuwa kaka zangu wawili walikuwa tayari wako sekondari hivyo ilinibidi kusubiri, ili wazazi waweze kujikusanya kiuchumi!

Nilijiunga na Shule ya sekondali Ukombozi iliyoko huko Urambo na nilisoma kwa muda wa mwaka mmoja tu nikaacha na kujiunga na Sekondari ya Mtakatifu Tomasi wa Akwino iliyoko Igunga-Tabora. Shule hii nilitafutiwa na aliyekuwa Paroko wa Parokia ya Urambo wakati huo Padre Athanas Kiyenze. Nilimaliza kidato cha nne 2002 na kufanikiwa kujiunga na Shule ya Sekondari ya Bihawana iliyoko Dodoma kwa masomo ya kidato cha tano na cha sita.

Maisha yangu ya wito

Hamu yangu ya utumishi katika shamba la Bwana imeanzia mbali kidogo kwa kuwa Baba yangu Modest Malale alikuwa Katekista kwa muda mrefu hivyo siku zote nikiwa bado mdogo nakumbuka jinsi nilivyokua natamani na mimi kuwa Padri siku moja. Hamu hii ilikolezwa na muziki ambao nilipenda kujifunza na kuimba. Nilipenda kujishughulisha na makundi ya vijana katika kwaya na maigizo Kanisani na hata nilipomaliza kidato cha sita niliendelea kuwa mwenyekiti wa Umoja wa Vijana Wakatoliki wa Jumuiya ya Mtakatifu Yuda Tadei (Kigamboni-Dodoma).

Baada ya masomo ya kidato cha sita nilituma maombi katika mashirika mbalimbali ya kitawa na kazi za kitume na kualikwa na Shirika la Wakarmeli kule Morogoro kwenda kuangalia maisha yao ili niamue kusuka au kunyoa!. Niliyaona maisha yao na kupendezwa nayo hivyo nikajiunga rasmi mwaka 2006. Nilifanya malezi ya upostulanti katika nyumba yetu iliyoko katika Parokia ya Malolo-Mikumi. Baada ya malezi hayo nilikwenda Lilongwe-Malawi kwa malezi ya Unovisi. Nilifunga nadhiri za muda mwaka 2008 kule Morogoro ambako niliendelea na masomo ya Falsafa katika Chuo cha Salvatorian pale pale Morogoro, ambacho kwa sasa ni Chuo Kikuu kishiriki cha Yordan.

Nilipomaliza masomo ya falsafa mwaka 2011 nilitumwa hapa Roma kuendela na masomo ya Taalimungu katika Chuo chetu cha kimataifa cha Mtakatifu Yohane wa Msalaba kilichopo ndani ya Chuo Kikuu cha Kipapa cha Teresianum. Tarehe 14/12/2013 nilifunga nadhiri za daima hapa hapa Teresianum na tarehe 5/04/2014 nategemea kupewa daraja la Ushemasi katika Kanisa kuu la Mtakatifu Pancras hapa Roma. Nawashukuru wote ambao wameendelea kunisindikiza kwa sala na majitoleo yao Mungu awabariki sana.

Utume wa Shirika nchini Tanzania

Shirika letu la Karmeli nchini Tanzania lipo katika Majimbo matano ambayo ni Jimbo kuu la Dar es Salaam, Jimbo kuu la Songea, Morogoro, Mbeya na Bunda. Karama yetu ya Shirika ni Sala na kazi za kitume! Tunajishughulisha na kutoa mafungo hasa katika nyumba yetu ya mafungo kule Mbeya na pia tunajishughulisha na maendeleo ya kielimu kama kozi za Saikolojia pale Morogoro, shule za Sekondari na msingi, Chuo cha Ufundi pamoja na kuendesha miradi midogo midogo ya kimaendeleo. Makao makuu yetu huko Tanzania yako Kihonda-Morogoro.

Historia ya shirika (Shirika la Mama Bikira Maria wa Mlima Karmeli)

Historia ya Shirika la Wakarmeli linaloundwa na Wanashirika wa kiume na wa kike pamoja na utawa wa tatu yaani Walei, inaanzia katika Mlima Carmeli kule Israeli ambako kundi la Wakaa pweke katikati ya karne ya kumi na mbili waliokuwa wakikaa mapangoni wakitafari na kusali liliamua kuomba kanuni ya maisha ili liweze kuishi maisha ya kitawa kama jumuiya. Mapokeo yanamtambua kwamba Mtakatifu Eliya kuwa ndiye Baba wa Shirika hili kutokana na uwepo wake katika mlima huu.

Mnamo mwaka 1209 Patriaki Albert wa Yerusalem aliwapatia kanuni ya maisha ya kitawa na kulingana na mapokeo ya ulinzi wa Mama Bikira Maria Jumuiya hii ikaitwa Shirika la Mama Bikira Maria wa Mlima Karmeli. Mwaka 1247 Baba Mtakatifu Innocenti IV aliwapatia kanuni iliyorekebishwa. Shirika lilianza kuenea maeneo mbali mbali baada ya Wanashirika hao kuja Ulaya na maeneo mengine.

Katika karne ya kumi na sita Mtakatifu Teresa wa Avila kule Hispania aliamua kuyafanyia marekebisho maisha ya watawa wa kike na baadaye kwa msaada wa Mtakatifu Yohana wa Msalaba waliweza pia kuyarekebisha maisha ya watawa wa kiume yaendane na maisha ya awali ya wakaa pweke waliokuwa wakijibidisha zaidi katika sala, tafakari ya Neno la Mungu na shughuli za kitume.

Watakatifu hawa wawili ndio hasa wanaobeba dhamana ya uanzilishi wa Shirika. Shirika hili kwa sasa lipo katika nchi 94 duniani makao makuu yake yakiwa hapa Roma na katika Afrika tupo katika nchi za Tanzania, Kenya, Uganda, Malawi, Rwanda, Burundi, DRC, Zambia, Nigeria, Afrika ya Kati, Afrika Kusini, Cameroon, Misri, Ghana, Ivory Cost, Visiwa vya Madagasca na Re-Union.








All the contents on this site are copyrighted ©.