2014-04-03 11:52:04

Mshikamano wa kidugu uwe ni dira na mwongozo wa ushirikiano kati ya Afrika na Ulaya


Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Bwana Ban Ki-Moon katika hotuba yake ya ufunguzi wakati wa mkutano kati ya Umoja wa Ulaya na Umoja wa Afrika huko Bruselles, tarehe 2 Aprili 2014 amekazia umuhimu wa Jumuiya ya Kimataifa kujikita katika mchakato unaopania kudumisha amani na usalama; maendeleo ya uchumi na kijamii pamoja na kuibua mikakati ya maendeleo endelevu kwa siku za usoni.

Kuna haja kwa viongozi wa Ulaya na Afrika kushirikiana kwa pamoja katika mchakato wa kuwajengea uwezo wanawake; kukuza na kudumisha usawa pamoja na kuwasikiliza vijana. Kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kujemga uwezo wa kuwa na uhakika wa usalama wa chakula kwa wote sanjari na kupambana na udhibiti wa athari za mabadiliko ya tabianchi kadiri ya mikakati iliyopangwa na Jumuiya ya Kimataifa.

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa anasema, uhamiaji na mikakati ya maendeleo endelevu ni kati ya changamoto zinazoikabili Jumuiya ya Kimataifa kwa sasa sanjari na kuhakikisha kwamba, haki msingi za binadamu zinalindwa na kuheshimiwa. Katika shughuli zote hizi, mshikamano wa kidugu unapaswa kuwa ni dira na mwongozo wa Jumuiya ya Kimataifa, ili kulinda na kudumisha utu na heshima ya kila binadamu.







All the contents on this site are copyrighted ©.