Papa Francisko kukutana na Malkia Elizabeth II mjini Vatican
Malkia Elizabeth wa pili anatarajiwa kukutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko,
Alhamisi tarehe 3 Aprili 2014. Hii itakuwa ni mara ya kwanza kwa Malkia Elizabeth
kukutana na Papa Francisko tangu alipochaguliwa kuliongoza Kanisa Katoliki, mwaka
mmoja uliopita. Katika Ibada ya Misa Takatifu iliyoadhimishwa na Baba Mtakatifu Francisko
hapo tarehe 19 Machi 2013, Uingereza ilituma ujumbe kuwakilisha katika tukio hili.
Malikia
Elizabeth atakuwa Italia kwa mwaliko kutoka kwa Rais Giorgio Napolitano wa Italia.
Ratiba inaonesha kwamba, Malkia pamoja na ujumbe wake, watapata chakula cha mchana
kwenye Ikulu ya Italia na baadaye jioni anatarajiwa kukutana na Baba Mtakatifu.
Rais
Napolitano alikwishawahi kutoa mwaliko kwa Malkia Elizabeth wa Uingereza kumtembelea,
tangu mwaka jana, lakini ilishindikana kutokana na sababu za kiafya. Kumbe, ziara
hii inalenga kutekeleza mwaliko kutoka kwa Rais Napolitano pamoja na kukutana na Baba
Mtakatifu Francisko.
Kumbu kumbu zinaonesha kwamba, Malkia Elizabeth wa Uingereza
alibahatika kukutana na kuzungumza na Mwenyeheri Yohane Paulo II mjini Vatican kunako
tarehe 17 Oktoba 2000 wakati wa Maadhimisho ya Jubilee ya Miaka Elfu mbili ya Ukristo.
Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI alikutana na kuzungumza na Malkia Elizabeth
wa Uingereza mjini London, wakati wa hija yake ya kitume iliyofanyika mwezi Septemba
2010. Kumbu kumbu zinaonesha pia kwamba, Malkia Elizabeth aliwahi kukutana na Papa
Yohane wa XXIII kunako Mwaka 1961.