Mataifa makubwa yanavyomezea utajiri wa Bara la Afrika!
China na Japan ni kati ya mataifa makubwa yanayoendelea kunyemelea utajiri wa rasilimali
kutoka Barani Afrika, China ikiongoza kwa kuwekeza kwa wingi zaidi na sasa Japan imeanza
pia kuamka. Safari ya kikazi barani Afrika iliyofanywa mwezi Januari na Waziri mkuu
wa Japan Shinzo Abe, ulikuwa ni mwanzo wa Japan kutaka kuwekeza katika nishati Barani
Afrika. Hii ni vita ya kidiplomasia na safari ya utafutaji wa nishati ya mafuta Barani
Afrika kama vyombo vya habari vinavyofafanua hali hii nchini Japan.
Waziri
mkuu wa Japan Shinzo Abe, katika safari yake ya kikazi, alitembelea Pwani ya Pembe.
Ethiopia na Msumbiji ambako hivi karibuni kumegunduliwa madini yanayoweza kutumika
katika nishati kwa kipindi cha miaka ishirini. Japan inataka kuwekeza katika nishati
nchini Msumbiji kwa kushirikiana na Brazil. Mradi wa "Pro Savana umepewa ekari millioni
kumi na moja za ardhi kwa ajili ya kilimo cha nafaka. Japan pamoja na mambo mengine
inataka pia kuwekeza katika nishati na miundo mbinu kama sehemu ya mchakato wa maboresho
ya maisha ya wananchi wa Msumbiji.
Wachunguzi wa mambo wanasema, kuna raia
millioni moja kutoka China wanaoishi na kufanya kazi Barani Afrika na kwamba, wamewekeza
kiasi kikubwa cha fedha katika shughuli za uzalishaji, ikilinganishwa na Japan. Lakini,
Japan inataka kuongeza kasi katika uwekezaji Barani Afrika na tayari katika kipindi
cha miaka mitano itatoa kiasi cha dolla za Kimarekani billioni mbili zitakazolipwa
kwa riba kidogo, ili sekta ya binafsi iweze kupata uwezo mkubwa zaidi wa kiuchumi.
Mambo
si haba kutokana na kugunduliwa kwa nishati Barani Afrika kwani hata nchi za Ulaya
zinamezea mate nishati na madini kutoka Barani Afrika, kama ambavyo hivi karibuni
Kampuni ya mafuta ya Total kutoka Ufaransa imetiliana sahihi mkataba na Serikali ya
Uganda tayari kuanza biashara ya mafuta kutoka Uganda. Ni matumaini ya wananchi wa
Bara la Afrika kwamba, wataweza kufaidika na rasilimali hii inayogambaniwa na Mataifa
makubwa duniani.