Jrs, Syria mshindi wa tuzo ya amani kwa Mwaka 2014
Shirika la Kitume Kimataifa la "Pax Christi" limelitunukia Shirika la Wayesuit la
kuhudumia Wakimbizi, Syria, Jrs, tuzo la amani kwa Mwaka 2014 kutokana na mchango
wake mkubwa katika kuwahudumia wakimbizi na watu wasiokuwa na makazi maalum nchini
Syria tangu mwaka 2011, vita ilipofumuka nchini Syria.
Tuzo hili lilianzishwa
kunako Mwaka 1988 kutokana na Mfuko wa Amani wa Kardinali Bernardus Alfrink na unatoa
tuzo kwa kuthamini mchango unaotolewa na watu binafsi, vikundi na mashirika mbali
mbali katika mchakato wa kulinda na kudumisha: haki na amani sehemu mbali mbali za
dunia.
Shirika la Wayesuit la kuhudumia Wakimbizi tangu mwaka 2008 limekuwa
mstari wa mbele katika kuwahudumia wakimbizi na wahamiaji kutoka Kaskazini mwa Afrika
na huko Mashariki ya Kati. Kwa namna ya pekee, kunako Mwaka 2001, Jrs ilijielekeza
zaidi kwa ajili ya kuwahudumia wakimbizi na wahamiaji kutoka Syria, kwa kutoa huduma
ya tiba, elimu na maendeleo. Jrs linaendesha pia kampeni ya haki, amani na upatanisho
wa kitaifa.
Jrs kwa sasa linaendelea kutoa msaada wa chakula kwa maelfu ya
wahamiaji na wakimbizi kutoka Syria pamoja na kuwapatia msaada wa tiba na elimu kwa
watu zaidi ya 9, 800. Kuna jumla ya watu laki tatu wanaohudumiwa na Jrs kutoka Syria.
Tuzo hii itatolewa hapo tarehe 8 Juni 2014 huko Sarayevo.