2014-04-01 08:03:53

Watu waguswe na Neno la Mungu!


Neno la Mungu linapaswa kuwafikia Watu wa Mataifa, ili waweze kulitafakari na hatimaye kulimwilisha katika maisha na vipaumbele vyao. Neno la Mungu ni dira na taa ya maisha ya waamini. Kuanzia tarehe 2 Aprili hadi tarehe 22 Juni 2014 kuna onesho la Maandiko Mtakatifu mjini Vatican, kufuatia onesho kama hili lililofanyika kunako mwaka 2012, ilikiongozwa na kauli mbiu "Verbum Domini" Yaani, Neno la Mungu. Onesho la Mwaka huu limesheheni utajiri mkubwa wa tafsiri za Biblia zaidi ya 200, ambazo zimepangwa kadiri ya maeneo ya kijiografia, kuonesha jinsi ambavyo Biblia imekuwa ni dira na mwongozo wa mataifa mengi duniani.

Monsinyo Lechior Sànchez de Toca y Alameda, Katibu mkuu msaidizi, Baraza la Kipapa la Utamaduni anasema, moja ya changamoto kubwa zinazoendelea kuwakabilia waamini wa nyakati hizi ni kutoifahamu Biblia. Biblia ni Maktaba yenye mkusanyo mkubwa wa vita ambayo kimsingi ingepaswa kufundishwa kwa umakini mkubwa shuleni kwani ni matokeo ya tamaduni na historia ya watu.

Kwa upande wake Kardinali Gianfranco Ravasi anasema, Biblia ni matunda ya tamaduni kwa maana kwamba, ni kanuni iliyochangia kwa kiasi kikubwa kukua na kushamiri kwa tamaduni za Mashariki. Ni matumaini ya Baraza la Kipapa la Utamaduni kwamba, watu wataendelea kuwa na kiu pamoja na njaa ya Neno la Mungu.

Wataalam wa masuala ya Maandiko Matakatifu wanabainisha kwamba, Neno la Mungu lina nguvu ya kuweza kupenya katika maisha na undani wa watu. Jambo linalofurahisha ni kuona jinsi ambavyo nguri wa Maandiko Mataktifu walivyofurahia kusoma, kutafakari na kulimwilisha Neno la Mungu katika vipaumbele vya maisha yao ndani na nje ya Kanisa. Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na sita, aliwahi kusema kwamba, Biblia ni Kisakramenti.

Neno la Mungu linapotangazwa katika Ibada na Liturujia, ni mwaliko wa kujibidisha kumfahamu Yesu Kristo anayezungumza na watu wake kwa njia ya Maandiko Matakatifu. Biblia kama Kisakramenti cha Kanisa ni kielelezo hai cha Neno la Mungu anayezungumza na binadamu katika historia ya maisha yake ya kila siku.

Onesho la Biblia ni mkusanyiko wa Biblia kutoka katika Maktaba za Kitaifa na zile za watu binafsi. Ni utajiri mkubwa wa Maandiko Matakatifu, yaliyoandikwa kwa ufundi mkubwa katika karatasi maalum, leo hii ndiyo Injili kama ilivyoandikwa na Luka pamoja na Yohane. Kwa kitaalam Maandiko haya yanajulikana kama "Papiro Bodmer 14 - 15". Kuna Biblia iliyoandikwa kwa mkono kunako karne ya IV ijulikanayo kama "Codex Vaticanus". Huu ni ushuhuda wa jitihada za makusudi kabisa katika kuhifadhi Maandiko Matakatifu.







All the contents on this site are copyrighted ©.