2014-04-01 06:57:43

Mambo yanayovuruga amani nchini Tanzania


Ukweli utawaweka huru ndiyo kauli mbiu inayoongoza ujumbe wa Kwaresima kwa Mwaka 2014 kutoka Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania. Katika ujumbe huu, Maaskofu wanapembua maana ya wongofu wa kweli unaowaweka huru; wajibu wa kuuishi, kuulinda na kuusimamia ukweli kishuhuda. RealAudioMP3

Baraza la Maaskofu Katoliki limeangalia hali halisi ilivyo nchini Tanzania. Sehemu hii ya mwisho, tunapenda kukushirikisha mambo yanayovuruga amani na utulivu nchini Tanzania, kama yalivyobainishwa na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania katika ujumbe wao wa Kwaresima.
Uvunjifu wa amani

Taifa letu linazidi kupoteza tunu bora ya amani ambayo waasisi wa taifa letu wametuachia. Katika siku za karibuni yamekuwepo matukio ya mauaji, watu kumwagiwa tindikali kwa sababu ya imani yao au visasi na hata mauaji kwa kutumia mabomu. Uhasama wa kidini na matukio ya kijasusi na ugaidi dhidi ya raia yanaonekana kushamiri. Kumekuwapo na matumizi makubwa ya nguvu upande wa vyombo vya dola vikitumia silaha za moto na za kivita. Wimbi la wananchi kutotii sheria na taratibu za nchi linakua. Tunakwenda wapi?

Amani lazima ilindwe ndani na nje ya mipaka ya nchi yetu. Hata hivyo, amani sio tunu inayojitegemea peke yake kwa kuwa amani ya kweli inazaliwa ndani ya mioyo yenye kujali misingi ya utu, haki, heshima, ukweli na umoja. Fikra tofauti na hizo, huzaa mioyo potofu, na mioyo potofu haiwezi kutoa amani.
Rushwa na madawa ya kulevya

Mapambano dhidi ya rushwa na madawa ya kulevya yamegeuka kuwa wimbo unaochosha kwa sababu hakuna dhamira ya dhati ya kuitokomeza. Uongozi wa juu unapotamka hadharani kuwafahamu watoa rushwa, wapokea rushwa na wafanyabiashara wa madawa ya kulevya lakini hakuna hatua zozote zinazochukuliwa ni hali inayotisha sana. Wakati umefika ambapo lazima tuwe wakweli kuhusu mapambano dhidi ya rushwa na madawa ya kulevya. Hatuwezi kuwa huru kuhusu rushwa na madawa ya kulevya kama hatujawa wakweli kuhusu mapambano dhidi ya rushwa na madawa ya kulevya. Wanaopiga vita rushwa majukwaani, ndio wanaoomba na kupokea nje ya jukwaa. Isitoshe rushwa ndiyo ngazi waliyoitumia na wanayoitumia kufika jukwaani. Katika mazingira kama haya hatujengi Taifa bali tunalibomoa na historia itatuhukumu. Hatuna budi kuunda misingi imara ya utawala bora. Tukumbuke daima kuwa utawala bora bila uwajibikaji na kuwajibishana ni kiini macho.
Kukua kwa matabaka katika jamii

Tofauti kubwa sana za kiuchumi zinazidi kupanua utengano wa kimatabaka kati ya wenye nguvu za kiuchumi na wasio na kitu. Wenye nguvu kiuchumi sasa wanamiliki uchumi, wanamiliki siasa na hatima ya fukara, na kwa fedha wananunua haki ya wanyonge.


Mgawanyo mbovu wa rasilimali za nchi unatisha. Ardhi inamilikiwa na wachache kwa kivuli cha uwekezaji mkubwa huku wananchi wakiahidiwa ajira kwa kuwa vibarua kwenye mashamba hayo badala ya kuwezeshwa kumiliki ardhi na kuitumia kwa faida. Haya ni masuala yanayomtia hofu mtu yeyote anayejali na kuthamini mustakabali wa taifa letu.
Siasa kuingilia weledi

Tatizo la siasa kutawala mifumo ya ujenzi wa misingi ya maendeleo linakua kwa kiwango cha kutia hofu. Kwa mfano, siasa na wanasiasa wanaathiri mfumo wa utoaji wa elimu nchini kiasi cha kulifanya taifa hili kuwa kama taifa lisilojali mustakabali wake. Yamekuwepo maneno mengi na mipango ya zimamoto isiyofanyiwa utafiti wa kina na utendaji umekuwa hafifu sana. Uthabiti katika kusimamia utekelezaji wa mipango ya maendeleo hauonekani na badala yake porojo zimetawala. Imejitokeza hali ya wale waliopewa dhamana ya kusimamia masuala ya elimu kwa mfano kukosa unyenyekevu wa kuwasikiliza na kushauriana na wataalamu katika nyanja hizi. Kila mara zinaibuka sera ambazo msingi wake ni ubunifu usiozingatia weledi na hivi kuifanya elimu kudidimia.
Mchakato wa Katiba mpya

Katiba kama moyo wa taifa ni chombo kinachopaswa kutengeneza misingi ya mfumo wa maisha mazima na uhai wa Taifa letu. Ukweli wote na uhuru wote wa Taifa unabebwa na Katiba. Iwapo mchakato wa katiba mpya hautaendeshwa kwa ukweli na uhuru, hatutaweza kupata katiba yenye kubeba ukweli na uhuru wote kuhusu taifa letu. Tunarudia tena kutamka kuwa zoezi hili adhimu na la muhimu kwa mustakabali wa Taifa limeharakishwa mno. Sasa tunaona zoezi zima limehodhiwa na wanasiasa. Mchakato wa katiba mpya unadai kuwepo kwa fadhila ya kijamii ya kutafuta manufaa ya wote (common good). Katiba si mali ya wanasiasa bali ni mali ya wananchi. Tunapenda kuialika jamii yote kuitendea haki nchi yetu. Tukae chini na tuzipime kila hatua zetu katika zoezi hili na tuone kama zinakidhi kipimo cha «Hekima, Umoja na Amani». Hekima ituongoze kulinda umoja wa Taifa letu na utuepushe na kishawishi cha kubaguana na kutengana. Kwa kuzingatia hilo umoja huo utatuongoza katika njia ya amani.

Uharibifu wa mazingira

Tishio kubwa la kimaangamizi kwa vizazi vijavyo linatokana na ukweli kuwa kumekuwepo na uharibifu mkubwa wa mazingira. Maendeleo yanagharama yake. Kiu ya kweli ya maendeleo ni lazima iambatane na ulazima wa kuwa makini katika kutunza mazingira na uthabiti wa uumbaji. Vyanzo vya maji na kingo za mito zimeharibiwa kwa kuruhusu shughuli za kilimo kufanyikia maeneo hayo, kwa kuruhusu makazi ya watu, viwanda kujengwa na kuruhusu takataka ya sumu kutoka viwandani na migodini kutiririkia kwenye vyanzo vya maji, nk. Ukataji wa miti umeshamiri na baadhi ya misitu ya asili imepotea. Kwa sababu hiyo tumechangia sana katika kusababisha mabadiliko ya tabia nchi ambayo athari zake sasa zinajionesha waziwazi. Ukame, njaa, mafarakano kati ya wakulima na wafugaji na kuenea kwa jangwa ni vitisho vilivyo dhahiri mbele yetu. Huu ni ukweli kuwa tumeshindwa kuzingatia agizo la Mungu la kuitawala na dunia kuutiisha ulimwengu. Tunahitaji sasa kubadilika ili ukweli utawale, tupate uhuru kamili kwa kuwajibika kuyalinda na kuyatunza mazingira kwa faida ya kizazi cha sasa na vizazi vijavyo.
Ni wajibu wetu Waamini Wakatoliki kuulinda ukweli na kuusimamia kiushuhuda. Jitahada za namna hii zina gharama yake kwa kuwa zinahitaji ujasiri wa kinabii na utayari wa kuteseka na hata ikibidi kutoa sadaka kubwa ya uhai.
HITIMISHO

Wapendwa Taifa la Mungu, tunapenda kuwahimiza kwa maneno haya tukisema: “Inunue kweli, wala usiiuze. Naam, hekima na mafundisho na ufahamu” (Mith 23:23). Ukweli ni msingi wa lazima na unapaswa kuwa wa kudumu kwa tendo lolote ili liweze kuitwa kuwa ni adilifu. Ukweli unapaswa kuzijenga dhamiri zetu ili kumsaidia mwanadamu kupata mwanga unaofukuza mikanganyiko.


Katika ulimwengu usiojali ukweli, uhuru unapoteza msingi wake na mwanadamu anakuwa mhanga wa vurugu ya vionjo na kutawaliwa kwa hila, iliyojidhihirisha waziwazi au iliyojificha. Hivi ni mwaliko kwetu sote “tuishike kweli katika upendo na kukua hata tumfikie yeye katika yote, yeye aliye kichwa, Kristo” (Efe 4:15). Kwa sababu upendo “haufurahii udhalimu, bali hufurahi pamoja na kweli” (1Kor 13:6).
All the contents on this site are copyrighted ©.