Wakimbizi kutoka Somalia wanaohifadhiwa nchini Kenya watalazimika kukaa kwenye kambi
mbili maalum zilizotengwa kwa ajili ya wakimbizi. Hayo yamebanishwa hivi karibuni
na Waziri wa mambo ya ndani wa Kenya Bwana Joseph Ole Lenku kama sehemu ya mchakato
wa kudhibiti mashambulizi ya kigaidi yanayoendelea kutishia maisha na usalama wa wananchi
wa Kenya.
Kikundi cha Kigaidi cha Al Shabaab chenye makao yake makuu nchini
Somalia, kimekuwa kikiendesha mashambulizi ya kushutukiza nchini Kenya na hivyo kusababisha
hofu na wasi wasi mkubwa nchini humo. Tangu sasa wakimbizi kutoka Somalia watalazimika
kuishi kwenye Kambi Dadaab na Kakuma. Kuna zaidi ya wakimbizi laki nne wanaoishi kwenye
Kambi la Daab na wengine 125, 000 wanaishi kwenye Kambi ya Kakuma.