Ratiba elekezi ya Hija ya kitume ya Papa Francisko Nchi Takatifu
Ili wote wawe wamoja ndiyo kauli mbiu inayoongoza Hija ya kitume ya baba Mtakatifu
Francisko katika Nchi Takatifu kuanzia tarehe 24 hadi tarehe 26 Mei 2014, kama sehemu
ya Maadhimisho ya Jubilee ya Miaka 50 tangu Papa Paulo VI alipokutana na kusali pamoja
na Patriaki Anathegoras wa Yerusalemu, tarehe 5 Januari 1964.
Baba Mtakatifu
anatarajiwa kuondoka mjini Roma, Jumamosi, tarehe 24 Mei 2014 majira ya Saa 2:15 asubuhi
na kuwasili Amman, Jordani saa 7:00 mchana na baadaye yatafuatia mapokezi ya heshima
yatakayofanyika kwenye Jumba la Mfalme Al – Husseini majira ya Saa 7: 45. Baba Mtakatifu
anatarajiwa kukutana na kuzungumza na viongozi wa Serikali ya Yordani majira ya saa
8:20 na baadaye Saa 10: 00 anatarajiwa kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye uwanja
wa Kimataifa wa Amman. Jioni Baba Mtakatifu atatembelea kwenye eneo la Ubatizo wa
Yesu, Ng’ambo ya Mto Yordan. Baadaye atakutana na kuzungumza na wakimbizi, wahamiaji
na vijana walemavu.
Jumapili tarehe 25 Mei 2014, Baba Mtakatifu ataondoka kwa
Elkopta kuelekea Bethlehemu anako tarajiwa kuwasili majira ya saa 3:30 asubuhi na
kupokelewa Ikulu, atakapokutana na kuzungumza na Rais wa Palestina Bwana Abu Mazen
na baadaye atazungumza na viongozi wengine wa Palestina. Majira ya saa 5:00 mchana,
Baba Mtakatifu ataadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa la Pango la Mtoto
Yesu na kufuatiwa na Sala ya Malkia wa mbingu. Baba Mtakatifu atapata chakula cha
mchana na baadhi ya Famili za Kipalestina kwenye nyumba mpya ya Wafranciskani iliyoko
mjini Bethlehemu. Baadaye, Baba Mtakatifu anatarajiwa kufanya matembezi binafsi kwenye
Pango la Mtoto Yesu na baadaye kutembelea kambi ya wakimbizi ili kusalimiana na watoto
wanaohifadhiwa kambini hapo.
Baba Mtakatifu majira ya saa 10: 00 Jioni ataondoka
kwa Elkopta kuelekea kwenye Uwanja wa ndege wa kimataifa Ben Gurion, Tel Aviv na anatarajiwa
kuwasili saa 10: 30 na kupokelewa na viongozi wa Serikali ya Israeli. Majira ya Saa
11:15 jioni, Baba Mtakatifu ataondoka kwa Elkopta kuelekea mjini Yerusalemu na hapo
atakutana na kuzungumza kwa faragha na Patriaki Bartolomeo wa kwanza na hapo kwa pamoja
watatia mkwaju kwenye Tamko la Kiekumene. Saa 1:00 za usiku, kutafanyika mkutano wa
kiekumene kama kilele cha maadhimisho ya Jubilee ya Miaka 50 tangu Papa Paulo VI alipokutana
na Patriaki Anathegoras wa Yerusalemu. Baba Mtakatifu na ujumbe wake watapata chakula
cha usiku nyumbani kwa Patriaki Bartolomeo wa kwanza pamoja na Maaskofu wa Kanisa
Katoliki madhehebu ya Kilatini.
Baba Mtakatifu Francisko ataianza siku yake
ya tatu ya hija ya kichungaji, Jumatatu tarehe 26 Mei 2014 kwa kumtembelea Mufti mkuu
wa Yerusalemu. Atapata fursa ya kutembelea Eneo la Msikiti mkuu, na baadaye atakwenda
kuweka shada la maua kwenye Ukuta ulioko kwenye Mlima Herzl pamoja na kutembelea
Jumba la Makumbusho la Yad Vashem. Saa 4:45 ratiba inaonesha kwamba, Baba Mtakatifu
anatarajiwa kukutana na kuzungumza na viongozi wakuu wa dini ya Kiislam na baadaye
kukutana na Rais Shimon Peres majira ya Saa 5:45, kwenye Ikulu ya Israeli.
Baadaye,
Saa 7:00 mchana Baba Mtakatifu Francisko anatarajiwa kukutana na kuzungumza na waziri
mkuu wa Israel Bwana Benjamin Netanyahu na baadaye, jioni atamtembelea tena Patriaki
Bartolomeo wa kwanza. Akiwa kwenye Kanisa la Getsemani, atakutana na Makleri, Watawa
na Majandokasisi. Saa 11: 20 jioni Baba Mtakatifu anatarajiwa kuadhimisha Ibada ya
Misa Takatifu na viongozi wakuu wa Makanisa ya Kikatoliki Nchi Takatifu. Baadaye ataondoka
kwa Elkopta kuelekea mjini Tel Aviv tayari kuagana na wenyeji wake wa Israeli na hivyo
kuondoka kurejea tena mjini Vatican.
Kimsingi hii ndiyo ratiba elekezi ya
hija ya kichungaji ya Baba Mtakatifu Francisko kwenye Nchi Takatifu kuanzia tarehe
24 hadi tarehe 26 Mei 2014. Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican, itaendelea kukujuza
yale yatakayojiri katika hija hii ya sala na kiekumene.