Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amewasili
mjini London, Uingereza, kwa ziara rasmi ya siku tatu ya kidola, moja ya ziara nadra
sana kufanywa na viongozi wa nchi za nje nchini Uingereza. Rais Kikwete na ujumbe
wake aliondoka nchini Tanzania usiku Jumamosi, Machi 29, 2014, kuelekea London kwa
ziara hiyo ya siku tatu ambako atakuwa Mgeni Rasmi wa Serikali ya Uingereza.
Katika
ziara hiyo, Rais Kikwete ambaye ameambatana na Mama Salma Kikwete pia anafuatana na
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Mheshimiwa Bernard Membe, Waziri
wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Mheshimiwa Hussein Mwinyi, Waziri wa Uchukuzi
Mheshimiwa Harrison George Mwakyembe, Waziri wa Nishati na Madini Mheshimiwa Sospeter
Muhongo, Waziri wa Fedha Mheshimiwa Saada Makuya na Waziri wa Biashara, Viwanda na
Masoko za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Mheshimiwa Nassoro Mazrui.
Rais
pia anafutana na Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Kanali (mst) J. Simbakalia na Naibu Waziri
wa Mawasiliano, Sayansi na Tekolojia Mheshimiwa January Makamba. Baada ya ziara ya
Uingereza, Rais Kikwete atakwenda Brussels, Ubelgiji kuhudhuria Mkutano wa Wanne wa
Wakuu wa Nchi za Umoja wa Ulaya (EU) na Afrika – EU-Africa Summit - uliopangwa kufanyika
kwa siku mbili – Jumatano na Alhamisi, wiki ijayo kwenye Makao Makuu wa EU mjini Brussels.
Mkutano
huo ambao mada yake kuu itakuwa ni Umuhimu wa Kuwekeza katika Watu, Ustawi na Amani
utahudhuriwa na wakuu wa nchi wanachama wa EU na wale wa Afrika akiwamo Rais Kikwete.
Mikutano ya wakuu wan chi za EU na Afrika imefanyika mara tatu mpaka sasa kuanzia
na ule wa kwanza wa mwaka 2000 mjini Cairo, Misri ukifuatiwa na ule wa Lisbon, Ureno
mwaka 2007 na Tripoli, Libya mwaka 2010.
Hiyo itakuwa mara ya kwanza kwa Rais
Kikwete kuhudhuria mkutano huo tokea ashike mamlaka ya kuongoza Tanzania mwishoni
mwa 2005. Rais Kikwete pia ameombwa kuhuduria mikutano mingine kadhaa ambayo itafanyika
wakati wa Mkutano huo mkubwa.