Maaskofu Katoliki Tanzania kuanza hija ya kitume mjini Vatican:Tarehe 4-7 Aprili 2014
Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania kuanzia tarehe 4 hadi tarehe 7 Aprili 2014 watakuwa
na hija ya kitume na kikanuni mjini Vatican, hija ambayo kimsingi inapaswa kufanyika
walau kila baada ya miaka mitano.
Katika mahojiano
maalum na Radio Vatican, Padre Raymond Saba, Katibu mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki
Tanzania anasema kwamba, hija ya Maaskofu ni kielelezo cha mshikamano wa umoja wa
Kanisa la Kiulimwengu na Makanisa mahalia. Hii ni fursa kwa Maaskofu kutembelea na
kuhiji kwenye makaburi ya miamba wa imani; yaani Mtakatifu Petro na Paulo yaliyoko
mjini Vatican pamoja na kukutana na viongozi wa Mabaraza ya Kipapa.
Kilele
cha hija ya Maaskofu ni kukutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko, ili kwa
pamoja kuweza kujadili: maisha, utume, changamoto na matarajio ya Kanisa la Tanzania
kwa siku za usoni. Itakumbukwa kwamba, Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania lilifanya
hija ya kitume na kikanuni kwa mara ya mwisho kunako mwaka 2005, wakati Mwenyeheri
Yohane Paulo II alipokuwa amelazwa kwenye Hospitali ya Gemelli. Wao wakawa ni Maaskofu
wa mwisho kama Baraza kuweza kukutana na Papa Yohane Paulo II.
Padre Raymond
Saba anasema, kimsingi hija ya kitume inapania pamoja na mambo mengine kudhihirisha
imani kama Baraza la Maaskofu wa Tanzania wakiwa wameungana na Baba Mtakatifu Francisko.