2014-03-31 09:18:25

Kifo hakizoeleki, tubuni na kuongoka msijidanganye kwamba muda bado!


Askofu Telesphor Mkude wa Jimbo Katoliki Morogoro, mwishoni mwa juma ameongoza Ibada ya Misa takatifu kwa ajili ya mazishi ya aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Mara John Tuppa aliyefariki dunia hivi karibuni akiwa kazini. Askofu Mkude amewataka watu waliohudhuria mazishi hayo kufanya toba na wongofu wa ndani kama njia ya kuleta mabadiliko kwenye maisha yao.

“Ninawaomba kila mmoja mahali hapa afanye toba, awe mkweli, asifanye uchakachuaji... kila mtu kwa imani yake aache mabaya na atende mema kama ndugu yetu John Tuppa ambaye alijitoa na kufanya zaidi kwa ajili ya wengine,” alisema. Aliwataka watu wote wajihoji njia zao kama ni kamilifu, na kwamba ni kwa vipi wanawatendea watu wengine wanaohusiana nao iwe ni baba, mama, watoto au hata maofisini na kwenye biashara.

“Je mnawaongozaje watu katika ofisi zenu katika ngazi mbalimbali, iwe ni wizarani, mkoani, wilayani hadi kwa mtendaji wa kijiji? Je, unawafanyaje watu katika biashara unayofanya? Je unawadhalilisha kwa kuwauzia vitu vibovu? Je, unawauzia madawa ya kulevya?” alihoji Askofu Mkude. Aliwataka watu wote kila mmoja kwa imani yake waendelee kuuombea mchakato wa Katiba ili iweze kupatikana Katiba bora zaidi. “Tuna wajibu kama wacha Mungu tuwaombee wajumbe wa Bunge maalum ili kazi ile ifanyike sawa na mapenzi ya Mungu. Tusipowaombea watafanya vitu vya ajabu,” alisisitiza.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Mahusiano), Bw. Stephen Wassira aliwavunja mbavu waombolezaji waliofika kwenye mazishi ya aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Mara marehemu John Gabriel Tuppa yaliyofanyika nyumbani kwake Kilosa mjini, mkoani Morogoro.

Akitoa salamu za rambirambi kwa niaba ya wabunge wa mkoa wa Mara, Bw. Wassira alisema watu wote waliohudhuria mazishi hayo wanataka kwenda peponi lakini tatizo ni masharti yanayoambatana na hiyo safari. “Baba Askofu Mkude (Telesphor), ukiuliza nani anataka kwenda peponi, wote hapa watanyoosha mikono, lakini tatizo ni masharti yanayoambatana na safari ya kwenda huko peponi. Kila mtu anaona ugumu wa hayo masharti ukiwemo wewe Baba Askofu,” alisema huku umati uliokuwepo ukiangua vicheko.

Alisema kifo hakizoeleki wala hakizuiliki na kwamba hakuna anayeweza kuchakachua siri ya Mwenyezi Mungu kuhusu uhai wa maisha ya wanadamu. Aliwaombea wafiwa wapate faraja katika kipindi hiki kigumu.

Akizungumza na waombolezaji wakati wa ibada ya mazishi nyumbani kwa marehemu, Jumamosi, jioni Machi 30, 2014, Waziri Mkuu Mizengo Pinda alisema amemfahamu marehamu Tuppa tangu mwaka 1993 alipoteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya kwa mara ya kwanza.

“Marehemu Tuppa amekuwa mtumishi Serikalini kwa muda wa miaka 42 na katika muda wote huo, miaka 21 ya utumishi wake ameitumia akihudumia wananchi kama Mkuu wa Wilaya na Mkuu wa Mkoa. Alikuwa ni mtu mwema, aliyejali watu na wala hakuwa na tamaa za hovyo hovyo,” alisema Waziri Mkuu.

“Kumpoteza mume na baba ni mtihani mkubwa lakini mkimtumaini Mwenyezi Mungu mtafaulu,” alisema Waziri Mkuu na kuwasihi mjane wa marehemu Tuppa pamoja na watoto wasisononeke wanapopatwa na jambo na wala wasisite kumuona Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, yeye binafsi ama Rais Jakaya Kikwete kwa msaada zaidi.

Mazishi hayo yalihudhuriwa pia na Makamu wa Rais, Dk. Mohammed Gharib Bilal, baadhi ya mawaziri, wabunge wa mikoa ya Mara na Morogoro, wakuu wa mikoa mbalimbali, viongozi wa dini na viongozi wa vyama vya siasa.

Bw. Tuppa alizaliwa Januari mosi, 1950. Amewahi kuwa Mkuu wa Wilaya za Chunya, Mwanga, Bukoba, Muleba na Dodoma kabla ya kuteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Mara mwaka 2011. Ameacha mjane, watoto watano na wajukuu watano.








All the contents on this site are copyrighted ©.