2014-03-29 09:38:29

Unashangaa nini? Tazama!


Ninatumaini sisi sote tumewahi kuusikia msemo huu: “Funguka macho, Angalia!” Usemi huu hauna maana kwamba mmoja ni kipofu au amefumba macho yake na sasa anaambiwa ayafungue ili aweze kuona, la hasha bali ni “Kufungua Macho” ili kuweza kuona vyema mambo katika maisha. Mathalani, neno hili linaweza kutumika na wazazi wanaomwonya mtoto wao wa kike anayempenda mvulana mwenye matatizo labda ya kubugia unga, au wizi au hana maisha mazuri au mvivu na hataki kufanya kazi.

Mama mtu anaweza kumwangalisha bintiye na kumwambia: “Mwanangu, funguka macho. Je, huioni hali halisi ya maisha ya huyo kijana unayempenda? Angalia sana usije ukajitatiza. Utadhani umepata kumbe umepatikana!” Kwa hiyo, kuna upofu unaotibiwa hospitalini na mganga wa macho, lakini pia kuna upofu mkubwa unaokupotezea mwelekeo wa maisha, upofu unaokuzuia usiweze kuona hatari iliyo mbele unakoenda katika maisha, upofu ambao unakufanya usione na kuchukua uamuzi gani unaofaa wa kufuata. Maisha kwako yanakuwa giza. Unabaki kama kipofu unayeegemea ukuta, au mkongojo, au kuwategemea wazazi. Wakati kumbe mtu anayeona ni huru hamtegemei mtu yeyote yule.

Leo tutapambana na mganga mkuu wa tiba ya upofu wa macho wa aina hii ya pili. Tutapata mwongozo wa kujikwamua na upofu wa maisha kijumla. Mwinjili Yohane anatuletea kituko cha uponyi wa kipofu wa macho kwa namna kama ya tamthilia au mchezo wa kuigiza ili kutufafanulia vizuri maana ya upofu huo wa maisha na uponywaji unaofanywa na Yesu.

Yesu anajionesha kama mganga wa macho, mponyi wa upofu unaotuwezesha kuona vyema njia tunayosafiri katika maisha na kuchagua vyema maisha kadiri ya thamani zitakiwazo. Kuna usemi wa Yesu anaosema: “Pindi niko duniani, mimi ni mwanga wa ulimwengu. Yesu ni jua linalomeremeta na kutuangaza sote.” Kutokana na ukweli huo, Injili ya Yohane inafungua kwa neno hilo la mwanga: “Kulikuja nuru amtiaye nuru kila mtu, akija katika ulimwengu. Yohane mbatizaji hakuwa nuru, bali alikuja kuishuhudia tu ile nuru yenyewe.” (Yoh 1:7-9).

Kristo ni mwanga unaotuwezesha kuona vyema maisha kwa namna inayoipa maana ya maisha yetu. Injili hii daima ilikuwa inatumika jumapili ya leo katika safari ya wakatekumeni watakaobatizwa Jumamosi Kuu. Baada ya kuibuka toka kwenye kisima cha ubatizo wakawa wanaitwa walioangazwa, wanaomeremeta. Yaani wale waliokuwa wamepata zawadi ya mwanga toka kwa Kristu! Waliofunguliwa macho juu ya kuuona vizuri ulimwengu.

Yawezekana kabla yake walikuwa wevi, wadanganyifu, wachakachuaji, wala rushwa, lakini bila kujitambua kuwa ni vipofu wakapotea njia, wakawa wanapuyanga porini tu hata hawajui wanakoelekea. Sasa wanafuata Injili ya Kristo inayowafungua macho yao. Hali ambayo tunaweza kuipata hata sisi, tunapokosea, kufanya uchaguzi usiofaa katika maisha, anafika mmoja na kutufungua macho, anapotuambia “Angalia, Kaa chonjo, Jihadhari,” hapo tunashtuka kwani tungekosea halafu mapato yake yangekuwa mabaya. Huo ndiyo ufunguo wa kuelewa fasuli ya Injili ya leo.

“Yesu alipokuwa anapita alimwona kipofu tangu kuzaliwa.” Hatuambiwi jina la mtu huyo, bali anatajwa tu kuwa ni kipofu, anaweza kuwa mtu yeyote yule. Maana yake hiyo ni hali ya kibinadamu, ya mtu yule ambaye hajakutana na Yesu, amezaliwa kipofu. Mtu wa namna hiyo, hawezi hata kuhitaji mwanga au nuru, kwa sababu haufahamu ulivyo kwa sababu hajauona. Wakati mwingine tunaweza kusikia watu wakisema: Mume wangu haendi kabisa Kanisani kusali, na hana hata wazo la kusoma biblia au kusikiliza mazungumzo ya mambo ya dini. Au unakutana na mtu, anakuambia “mimi sina hamu kabisa na ukristo, yaani sina interest kabisa!”

Hilo si jambo la kushangaza, kwa sababu Mtu ambaye hajauona mwanga, (kipofu) hajakutana na Kristu, itakuwa ni kumdai mno mtu wa namna hiyo (kipofu) atamani kuutazama ulimwengu kwa namna tofauti. Kwa sababu hana wazo, hawezi kufikiri namna nyingine, hawezi kujua, ni kitu gani hiyo nuru. Mtu aina hiyo ni kipofu anahitaji kufunguka macho. Ni sawa na mtu anayekuja kugundua uhondo wa muziki, uhondo wa riadha, uhondo wa kufanya hija, uhondo wa kusoma hesabu, uhondo wa siasa, nk. Kabla yake hakuwa anashabikia chochote, sasa utamkuta anafurahia kwa sababu kuna mtu amemfungua macho – anakuwa limbukeni hana siri.”

Wanafunzi wa Yesu wanapomwona huyo kipofu wanakuwa kama waafrika mbele ya matatizo, wanaanza kumtafuta mchawi, wanamwuliza Yesu: “Rabi, ni yupi aliyetenda dhambi, mtu huyu au wazazi wake hata azaliwe kipofu?” Hebu angalia kwa makini jibu la Yesu ni tofauti kabisa na fikra zetu. Anajibu kifupi tu: Hiyo ni hali halisi ya maisha. Kwamba mtu anazaliwa hivyo. “Hiyo ni kazi ya Mungu.” Mwanga huu unatoka mbinguni, siyo jambo analoweza kulileta binadamu. Yawezekana akaendelea kuwa kipofu hivyo hadi kufa, au kuweza kubahatika kukutana na Kristu anayeweza kukufungua macho kwa neno lake.

Yesu hataki kusikia watu wanazungumza juu ya dhambi kama inavyozoeleka kusikia kwamba, dhambi imeingia duniani kwa njia ya wazazi wetu wa kwanza na hivi sisi sote tuko katika dhambi, la hasha, bali sisi tunazaliwa hivyo. Yesu anatualika kufunguka macho, kuangalia nuru ya Mungu daima, na ni yeye pekee anayeweza kutufungua macho na kuona ulimwengu kwa namna ya pekee.“Baada ya kusema hayo, Yesu alitema mate chini na kufanya tope kwa yale mate. Kisha akampaka kipofu kope za macho”. Tendo hilo ni muhimu sana, kwa vile inarudiwa kusemwa mara tano katika fasuli ya Injili ya leo Yesu alitema mate chini na kufanya tope kwa yale mate.

Tumeshasikia mara nyingi katika Agano la kale, juu ya tope, ya pumzi ya Mungu na mate. Hayo yanamaanisha uhai au uzima. Kitendo kilichofanyika cha Mungu alipomwumba Adamu. Yesu anakirudia kitendo hicho ikiwa kama ni uumbaji upya wa mtu mpya. Sasa mtu mpya anazaliwa kutokana na mwanga wa Kristu. Yaani sasa mtu anaishi kama inavyotakiwa kuwa binadamu. Anajua anakotakiwa kwenda kisha anamtuma huyo kipofu na kumwambia: “Nenda kanawe katika birika ya Siloamu, maana yake aliyetumwa.” Wataalamu wanasema Siloamu maana yake siyo aliyetumwa, neno kutumwa lingekuwa shaluak ambacho ni kisima pekee kilichokuwa katika mji ule wa Yerusalemu.

Hapa kwa neno hilo mwinjili anataka kuonesha maji yale ambayo yanamfungua macho, kama maji ya ubatizo, na yule ambaye anampa mwongozo wa kuyapata hayo maji yaani Roho wa Kristu, yaani maisha ya kimungu ambayo yanakuwezesha kuona hali halisi ya maisha. Baada ya kutoka kisimani kunafuata mfululizo wa vituko vinavyomsibu kipofu huyu aliyepona. Hiyo ni sawa na safari ya mtu anayeona mwanga baada ya kufunguliwa macho na Yesu. Mtu anayesafiri peke yake bila kutegemezwa na Yesu. Safari ya kipofu huyu ni sawasawa na safari yetu wakristu kuelekea mwanga. Unaalikwa kutanguzana kipofu huyu ujifunze kutembea vyema baada ya kupata mwanga wa ubatizo ili kuelekea kwenye mwanga halisi wa maisha.

Kulikuwa makundi kadhaa ya watu waliokuwa wanahoji na kuujadili uponyi wa kipofu huyu kwa namna yao. Kikundi cha kwanza alichopambana nacho huyu kipofu ambaye sasa anaona ni cha majirani waliokuwa karibu sana naye: Watu hao wanaonekana sasa kutokuwa na uhakika kama wanayemwona ndiye aliyekuwa kipofu mwombayala maskini au la, wanaulizana: “Je! Huyu siye yule aliyekuwa akiketi na kuomba? Wengine wakasema ndiye. Wengine wakasema, La! lakini amefanana naye.”

Tunaweza kujiuliza, je, kumetokea nini hadi Mtu huyu hatambulikani tena na jirani zake alioishi nao. Hiyo ndiyo historia ya maisha yetu, hiyo ni hali halisi ya maisha yetu. Historia ya wale waliokuwa vipofu ambao walikuwa wanatembea bila kuelewa wachukua uchaguzi gani mzuri wa maisha. Wanapofunguka macho katika nuru ya Kristu, wanakuwa watu tofauti kabisa hadi kutokutambulikana tena na watu aliozoeana nao kabla.

Yawezekana mtu alikuwa anathamini mambo mengine kabisa ya duniani, magari, nyumba, raharaha, lakini sasa amegundua thamani nyingine bora zaidi za maisha. Labda alikuwa mpiga rushwa, au mchakachuaji, mdanganyifu, sasa ni kinyume chake. Sasa amefunguka macho. Hivi unapokutana na wanaomfahamu, wanaweza kubishana wenyewe kwa wenyewe. Ni yule au siyo yule tunayemfahamu? Maana yake mtu aliyeangazwa kweli, anakuwa tofauti kabisa kwa sababu yuko katika safari kuelekea mwanga.

Wanapomwuliza Kipofu huyo anathibitisha kwamba ndiye: “Mimi ndiye”. Watu hao wanataka kujua “Kulikoni” wanamwuliza “Yalifumbukaje”. Naye anarudia kueleza ilivyokuwa: Mtu yule aitwaye Yesu alifanya tope akanipaka macho akaniambia, Nenda Siloamu ukanawe; basi nikaenda na kunawa, nikapata kuona”. Inakuwa vizuri sasa hata mimi ninapoulizwa swali la mtindo kama huo imekuwaje hadi uwe mkristu, ulipatapataje wito wa ukristo, wa utawa, wa ukatekista au upadre?

Kipofu anaendelea na safari yake ya maisha. Mara anakutana na kikundi cha pili cha watu ambao ni viongozi wa kanisa. Yaani watunzao mapokeo yadini na ambao tungetegemea wangestaajabia kumwona aliyekuwa kipofu sasa anaona. Kumbe hao wanachukizwa na mtu aliyemfungua macho kipofu huyu. Kikundi hicho cha pili siyo cha wengine bali ni cha Mafarisayo: Chuki yao inakuja pale wanapotambua kwamba, huyu kipofu kabla yake alikuwa anafuata amri zao, alikuwa anafanya wanachotaka wao, alikuwa amewategemea kumbe sasa amefunguka macho, anaona mambo kwa namna tofauti.

Hao ni maadui wa nuru, wanawawakilisha wale walio wafungwa wa fikra zao, dhana zao, mawazo yao juu ya Mungu. Wamefungwa katika utamaduni na mapokeo yao na hawataki kubadili kitu. Hapo wanasema mtu aliyemponya kipofu siyo mtu wa Mungu kwani hashiki sheria ya sabato ya mapokeo yetu. Hivi wanamhoji: “Mafarisayo nao wakamwuliza tena jinsi gani alivyopata kuona.” Naye kipofu anatoa majibu yaleyale aliyotoa mwanzoni: “Alinitia tope juu ya macho nami nikanawa, na sasa naona.” Wanapobishana wao kwa wao juu ya mtu huyo wanagawanyika na wanashindwa kupata jibu wanalolitaka, wanamwuliza tena kipofu mara ya pili, “Wewe wasemaje katika habari zake kwa vile alivyokufumbua macho?” Kipofu anatoa jibu linalompa cheo zaidi Yesu: “Mimi kwa binafsi yangu naona kuwa mtu huyu: ‘ni nabii’”.

Kikundi cha tatu ni wazazi wanaoitwa na wafarisayo na kuulizwa maswali: Wazazi wanamfahamu vizuri sana mtoto wao. Viongozi wanawauliza wazazi “Huyu ndiye mwana wenu, ambaye mnasema kwamba alizaliwa kipofu? Amepataje, basi kuona?” Wazazi wanaruka swali la pili na kulijibu la kwanza: “Tunajua ya kuwa huyu ndiye mwana wetu, tena ya kuwa alizaliwa kipofu; lakini jinsi aonavyo sasa hatujui. Wala hatujui ni nani aliyemfumbua macho. Sisi hatumo katika suala la kufunguka kwake macho. - Mwulizeni yeye mwenyewe, yeye ni mtu mzima, atajisemea mwenyewe.” Yaani alizaliwa kipofu, na kuna mwingine amemfungua macho”.

Hapa unaona kama vile wazazi hawa wanaogopa, wana woga wa kuponywa. Wanamwogopa kijana anayeona mambo kwa namna ya pekee kuliko namna ile waliyomfundisha wao. Wazazi wana wasiwasi, kwa sababu wale ambao hawafuati mapokeo wanaweza kufukuzwa toka hekaluni. Hapa unaweza kuwakumbuka watu ambao wametoa mchango mkubwa sana katika jamii, katika siasa lakini hawapokewi vizuri. Mwanga ni hatari, unagombanisha watu.

Kinakuja kikundi kingine cha nne ambacho ni kilekile tena cha mafarisayo, wanamwambia yule kipofu: “Mpe utukufu Mungu.” Ni sawa na kusema: “Umshukuru Mungu”. Maana yake, wewe kiri tu kwamba umekosea, kisha sisi tutajitahidi kuweka mambo sawa. Hasahasa kurekebisha kufuru hii iliyojitokeza kwa sababu “Sisi tunajua ya kuwa mtu huyo ni mwenye dhambi.”

Hapo kipofu anaanza kuitetea hali halisi anayojisikia kuwa nayo, yaani hali ya kuona mwanga mpya wa Kristu aliyemfungua macho hayo. Anawapa ukweli wao: “Kwamba yeye ni mwenye dhambi hilo mimi silijui. Najua neno moja, kuwa mimi nalikuwa kipofu na sasa naona.” Hapo tunajifunza kwamba yabidi kwa haki yote kujiacha kutetewa na matendo na siyo kwa sheria. Unaona wazi kuwa mtu huyu aliyepata mwanga sasa anazidi kuwa na uhakika zaidi wa mambo na kujiamini zaidi.

Wanapomwulizia tena jinsi alivyofumbuka macho wanapomwuliza: “Alikutendea nini? Alikufumbua macho jinsi gani?” Wanataka aendelee kujibu, ili waweze kutafuta mwanya wa kumkosoa. Hapo yule kipofu anawashtukia na kuwapa “makavu laivu”. “Nimekwisha kuwaambia, wala hamkusikia; mbona mnataka kusikia tena? Yawezekana labda na ninyi mnataka kuwa wanafunzi wake?” Ni kitu cha kawaida kutoa majibu haya makavu. Na kutoka hatua hii sasa wanaanza kutupiana lugha za kebehi na matusi ya rejareja. “Wewe ndiye mwanafunzi wake, sisi tu wanafunzi wa Musa. Sisi tunajua ya kuwa Mungu alisema na Musa; bali yule hatujui anakotoka.” Mafarisayo daima wanakimbilia kusema: “Sisi tunajua” na huyu kipofu daima anasema “Mimi sijui”. Watu wanaofikiri kwamba daima wanajua yote hawawezi kupata mwanga, watabaki daima kuwa katika giza.

Wafarisayo wanaposema kwamba hawajui anakotoka Yesu, kipofu anawakebehi tena na kuwaambia: “Hii ni ajabu! Ninyi mnaojua mambo yote, lakini hamumjui anakotoka huyu aliyenifumbua macho!” Ni kama anawaambia: “Tunakichojua sisi wenyeji yaani watu wa kawaida ni hiki kwamba, mcha Mungu (anayemwogopa Mungu) daima anasikilizwa na naye Mungu.

Aidha, haijawai kusikika kwamba kumetokea mtu anayafumbua macho ya mtu aliyezaliwa na hali ya kipofu. Asiyetoka kwa Mungu hawezi kutenda neno lolote.” Kutoka kwenye hali ya kebehi hadi wanafikia kukashifiana na kutoleana lugha chafu. Hawa wafarisayo, wanashindwa kuhimili vishindo wanaamua kumfukuzia nje. Ni namna dhahiri ya kutenda ya mtu asiyetaka kufunguka macho na kuuona mwanga. Ukifuatilia mazungumzo haya utaona jinsi yalivyopanuka kidogokidogo kutoka kwenye ushawishi, kebehi na dharau matusi hadi kuchefuana nyongo na mwisho kumfukuza mtu. Ndiyo mtindo wa kufanya mambo mtu asiyetaka kufunguka macho. Kipofu anaondoka, anajiona kuwa huru anatoka nje.

Katika sehemu ya mwisho ya Injili tunasikia kwamba yule kipofu akakutana tena na Yesu. Lakini ukweli ni kwamba Yesu alimtafuta yule kipofu ndipo walipokutana nje walikofukuziwa wote wawili. Yesu anaenda kumtafuta mwenzake ambaye naye amefukuzwa kama yeye. Anajua kuwa yule anayepokea mwanga, hawezi kutazamwa vyema na watu wa mapokeo. Yesu akamwuliza: “Wewe wamwamini Mwana wa Mungu?” Yaani wewe unajiaminisha kweli kwa mtu aliyekufungua macho? Yule kipofu anajibu “Ni nani, Bwana, nipate kumwamini?”. Yesu anamjibu: “Umemwona, unayesema naye ndiye.” Mtu aliyeangazwa hahitaji tena uwepo wa mwalimu. Alikuwa ameongozwa katika safari yake na ile Injili inayoendelea kumfungua macho. Ndugu yangu, katika safari yako ya maisha funguka macho uongozwe na nuru ya Kristo yaani Neno lake.
Alcuin Nyirenda, OSB.








All the contents on this site are copyrighted ©.