Sakramenti ya Mpako wa Wagonjwa si tiketi ya kuelekea kaburini!
Kwa njia ya Sakramenti za kuingizwa katika Ukristo, mtu hupokea uzima mpya wa Kristo
unaochukuliwa katika vyombo vya udongo nao hubaki umefichika pamoja na Kristo. Mwanadamu
yumo duniani akielemewa na hali ya mateso, magonjwa na kifo. Uzima mpya wa watoto
wa Mungu unaweza kudhohofika na hata kupotezwa kwa dhambi.
Mama Kanisa anafundisha
kwamba, Yesu Kristo ni mganga wa roho na miili; alisamehe dhambi na kuwarudishia watu
afya ya miili. Ni kwa njia ya utashi wa Yesu mwenyewe kwamba, Kanisa kwa nguvu ya
Roho Mtakatifu liendeleze kazi ya uponyaji na wokovu hata miongoni mwa viungo vyake.
Hili ndilo lengo kuu la Sakramenti za Uponyaji, yaani Sakramenti ya Kitubio na Mpako
wa Wagonjwa.
Kwa mpako mtakatifu wa wagonjwa na sala za makuhani, Kanisa lote
huwakabidhi wagonjwa kwa Bwana aliyeteswa na kutukuzwa ili awainue na kuwaokoa. Kanisa
linawahimiza wagonjwa kujiunga kwa hiari na mateso na kifo cha Kristo ili kuchangia
mafao ya Taifa la Mungu. Pamoja na Katekesi ya kina, waamini wengi wamekuwa na woga
wa kupokea Sakramenti ya Mpako wa Wagonjwa, wakidhani kwamba, hiyo ni tikeketi ya
kuwapeleka kaburini.
Baraza la Maaskofu katoliki Senegal kwa kutambua umuhimu
wa Sakramenti ya Mpako wa Wagonjwa, Jumapili tarehe 30, 2014 linafanya semina maalum
ili kutambua kwa mara nyingine tena umuhimu wa Sakramenti ya Mpako wa Wagonjwa, ili
waamini wengi waweze kukimbilia huruma na upendo wa Mungu katika mahangaiko yao wakati
wanapokuwa katika Altare ya mahangaiko ya binadamu. Sakramenti ya Mpako wa Wagonjwa,
ipewe hadhi yake hasa na wafanyakazi katika Sekta ya Afya na waamini katika ujumla
wao.
Siku hii inapambambwa kwa tafakari za kina kutoka kwa wadau mbali mbali
katika shughuli za kichungaji kwa wagonjwa, Ibada ya Misa Takatifu pamoja na Ibada
ya Kuabudu Ekaristi Takatifu.