2014-03-29 07:53:55

Ninyi mlioonja huruma ya Mungu, waonjesheni wengine huruma hiyo wala msiibinafsishe!


Baba Mtakatifu Francisko amewaongoza waamini kutoka sehemu mbali mbali za dunia kujiandaa kikamilifu kuadhimisha Jumapili ya nne ya kipindi cha Kwaresima, Jumapili inayojulikana kuwa ni Jumapili ya furaha, kwa: kufunga na kusali; toba na wongofu wa ndani; kuabudu Ekaristi Takatifu pamoja na kuungama dhambi zao. Kwaresima ni kipindi cha toba na wongofu wa ndani unaopaswa kuwa ni endelevu. Hii inatokana na sababu kwamba, hakuna mwanadamu anayeweza kujidai kwamba, ni mkamilifu, kumbe anajitaji kujipatanisha na Mungu pamoja na jirani.

Katika mahubiri yake kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Ijumaa jioni, Baba Mtakatifu amewaambia waamini kwamba, kuna mambo msingi ambayo waamini wanapaswa kuyazingatia katika maisha yao. La kwanza ni kujitahidi kuwa watu wapya kadiri ya mpango wa Mungu kwa kutambua kwamba, wao ni watoto wa Mungu, wafuasi wa Kristo na Kanisa wanaopaswa kugeuza mienendo yao kwa kukazia utu na heshima yao kama binadamu na wala si kwa utajiri alionao mtu!

Waamini wajitahidi kuyaangalia maisha yao katika mwanga wa neema kwa kutambua kwamba, moyo wa mwanadamu unaotekeleza mapenzi ya Mungu, utajitahidi kujielekeza katika kufuata ukweli badala ya kujikita katika majungu; kugawana mali na utajiri na wale ambao hawakubahatika badala ya kuiba na kujichimbia katika ufisadi; badala ya kuelemewa na chuki na hali ya kutaka kulipiza kisasi, mwamini ajitahidi kuwa mpole na mnyenyekevu wa moyo, tayari kusamehe na kusahau; badala ya kuendekeza majungu na umbea unaoharibu sifa njema ya watu, mwamini ajitahidi kuona mazuri kutoka kwa jirani zake.

Baba Mtakatifu anawaalika waamini kujikita katika upendo thabiti na udumifu kwani hii ni sehemu ya maisha ya Mwenyezi Mungu. Upendo unashinda dhambi na una nguvu ya kuweza kuanza tena upya kwa kusamehe, kama inavyojionesha katika sehemu ya Injili ya Baba Mwenye huruma, anayeacha daima mlango wazi, akimsubiri Mwana mpotevu ili aweze kurejea tena nyumbani kwa Baba, ili kushiriki tena huruma na upole wa Mungu, kwani Yeye ni chemchemi ya upendo na mwaliko wa kupenda kama anavyopenda Yeye.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, ushuhuda wa upendo unaotolewa na Wakristo sehemu mbali mbali unapaswa kuwa ni kielelezo cha wafuasi aminifu wa Yesu. Upendo una sifa ya kushirikisha wengine badala ya kujifungia katika ubinafsi. Kwa asili, upendo uko wazi na una tabia ya kujiongeza zaidi na zaidi. Baba Mtakatifu anawashukuru wote waliohudhuria Ibada hiyo na kwamba, kwa muda wa masaa ishirini na manne, wataweza kujipatanisha na Mungu pamoja na jirani zao. Hili ni tukio ambalo limewashirikisha waamini kutoka katika Majimbo na Parokia mbali mbali duniani.

Hii ni furaha ya kupokea huruma ya Mungu ili kujenga na kuimarisha urafiki, tayari kujimaga uwanjani kusherehekea zawadi ya maisha mapya. Baba Mtakatifu anasema, kwa yule anayeonja huruma ya Mungu anachangamotishwa hata yeye kuwa ni chombo cha huruma kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii. Waamini wataonja huruma kwa kuwaonjesha wengine huruma, ili hatimaye, kusherehekea Pasaka ya Bwana kwa furaha kubwa!







All the contents on this site are copyrighted ©.