2014-03-29 08:58:14

Mfuko wa Mshikamano Barani Afrika kunufaisha nchini 6 kwa sasa!


Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa, FAO limeanzisha Mfuko wa Mshikamano Barani Afrika, kama sehemu ya mchakato wa kuwa na uhakika wa usalama wa chakula Barani Afrika. Nchi ambazo zitakuwa za kwanza kufaidika na mfuko huu ambao umezinduliwa hivi karibuni huko Tunis, Tunisia ni: Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati, Ethiopia, Malawi, Mali, Niger na Sudan ya Kusini. Kila nchi iliyotajwa hapo juu itapatiwa kiasi cha Dolla Millioni mbili za Kimarekani kutoka katika Mfuko huo.

Akizungumzia juhudi hizi, Bwana Graziano da Silva, Mkurugenzi mkuu wa FAO anasema, nchi nyingi za kiafrika zimeonesha utayari wa kushirikiana na nchi majirani katika kujenga na kuimarisha mikakati ya usalama wa chakula kanda ya Bara la Afrika kwa kuwa na uhakika wa kesho iliyo bora zaidi. Mkataba huu umefanyika wakati wa mkutano wa FAO, Kanda ya Bara la Afrika uliohitimishwa hivi karibuni na kwamba, nchi mbali mbali za Kiafrika zinaalikwa kujiunga na Mfuko huu.

Fedha za Mfuko wa Mshikamano Barani Afrika zitatumika kugharimia miradi ya maboresho ya uhakika wa usalama wa chakula Barani Afrika, lishe, kilimo na maendeleo vijijini. Ni mradi inaopania kuongeza fursa za ajira miongoni mwa vijana; maboresho ya rasilimali za utawala bora na uzalishaji makini wa chakula; kuboresha hali ya maisha ya watu wanaoishi katika maeneo ya vita pamoja na kuhakikisha upatikanaji wa chakula.

Mfuko wa Mshikamano Barani Afrika unahifadhiwa na FAO na ulizinduliwa kunako Mwaka 2012 na kuzinduliwa na Rais Denis Sassou Nguesso, kutoka Congo Brazzaville.







All the contents on this site are copyrighted ©.