2014-03-29 07:56:13

Jitahidini kuwa ni mashahidi amini wa Kristo na Kanisa lake!


Baba Mtakatifu Francisko, Ijumaa tarehe 28 Machi 2014 amekutana na kuzungumza na Baraza la Maaskofu Katoliki Madagascar waliokuwa wanafanya hija yao ya kitume mjini Vatican, hija inayofanyika walau kila baada ya miaka mitano. Katika hotuba yake ambayo amewakabidhi Maaskofu kutoka Madagascar, Baba Mtakatifu amekazia umuhimu wa Mama Kanisa kuwa karibu zaidi na maskini pamoja na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii kutokana hali na nafasi zao katika Jamii.

Amewewahimiza Maaskofu na waamini katika ujumla wao, kuwa ni wajenzi na vyombo vya haki, amani na upatanisho nchini Madagascar pamoja na kuhakikisha kwamba, wanawajengea uwezo maskini ili waweze kupambana na hali yao ya maisha. Kanisa liwe mstari wa mbele anasema Baba Mtakatifu Francisko katika kulinda na kutetea tunu msingi za maisha ya ndoa na familia nchini Madagascar na kwamba, maisha ya waamini yawe ni kielelezo cha wafuasi waamifu wa Kristo na Kanisa lake kwa kuishi kadiri ya kweli za Kiinjili.

Baba Mtakatifu anawaambia Maaskofu na Mapadre kutoka Madagascar kwamba, wanapaswa kuchuchumilia toba na wongofu wa ndani, ili kweli maisha yao yaweze kuwa na mvuto na mashiko kwa watu wanaowahudumia, kwa kuendelea kuwa ni wafuasi aminifu wa Kristo na Kanisa lake. Wawe daima mstari wa mbele kutafuta: haki, amani, upendo na mshikamano wa kitaifa na mafao ya wengi. Kwa namna yoyote ile wasiwe ni sababu ya mgawanyiko wa kisiasa.

Baba Mtakatifu anawahimiza Maaskofu wa Madagscar kuwekeza zaidi katika sekta ya elimu, kama sehemu ya mchakato wa Uinjilishaji Mpya. Watoto wengi wenye umri wa kwenda shule, wapewe nafasi ya kusoma na kuendelea na masomo yao. Wanafunzi walelewe na kukuzwa mintarafu maadili, utu wema pamoja na tunu msingi za Kiinjili.

Wananchi wasaidiwe kujenga na kuimarisha umoja na mshikamano wa dhati miongoni mwa wananchi wa Madagascar; walinde na kutetea utu na heshima ya binadamu; wakuze utamaduni wa haki na amani, majadiliano na upatanisho wa kitaifa kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wananchi wa Madagascar kwa sasa na kwa siku za usoni.

Baba Mtakatifu anawapongeza Maaskofu wa Madagascar kwa kukazia majiundo makini ya wanandoa watarajiwa. Anasema, Familia ya binadamu inakabiliwa na vitisho pamoja na changamoto nyingi, kumbe haina budi kulindwa na kuendelezwa, ili kutoa mchango wake ndani ya Kanisa na Jamii katika ujumla wake, kwa kujenga watu wenye ukomavu wanaoweza kuchangia katika tunu msingi za maisha ya kijamii, haki na amani. Familia zisaidiwe katika hija ya maisha yake ya kiimani, ili ziweze kuwa kweli ni shule ya sala, tafakari ya Neno la Mungu na maisha ya Kisakramenti.

Baba Mtakatifu anaendelea kuhimiza majadiliano ya kidini na kiekumene kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi nchini Madagascar. Toba na wongofu wa ndani unaopata chimbuko lake katika Maandiko Matakatifu ni changamoto endelevu ili kufikia maisha ya uzima wa milele. Wakristo watolee ushuhuda wa imani yao kwa Kristo na Kanisa lake. Makleri na watawa watambue kwamba, wao ni vyombo vya huduma kwa Mungu na Jamii. Kanisa liwe makini kuteuwa vijana wanaoomba kujisadaka kwa ajili ya Upadre na Utawa. Wafundwe kuheshimu na kuthamini mashauri ya Kiinjili; makini katika matumizi ya mali ya Kanisa kama kielelezo cha Kanisa linalojali maskini na wanyonge.

Baba Mtakatifu anawaalika kwa namna ya pekee, Maaskofu kuwa karibu zaidi na Mapadre wao katika mahitaji yao ya kiroho na kimwili. Anasema anawakumbuka wote katika maisha na utume wao, kwa kujisadaka kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake hata katika mazingira magumu. Pamoja na changamoto zote za maisha, Mapadre wanapaswa kuwa karibu zaidi na waamini wao, ili kuwatangazia Injili ya Furaha. Maaskofu washirikiane na kushikamana na Mapadre wao ndani ya Kristo, ili kwa pamoja, waweze kweli kusambaza harufu ya furaha inayobubujika kutoka katika Injili ya Kristo.







All the contents on this site are copyrighted ©.