2014-03-29 09:16:59

Askofu Godfrey Mdimi Mhogolo wa Kanisa Anglikan, afariki dunia, Afrika ya Kusini


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Jakaya Mrisho Kikwete amemtumia Salamu za Rambirambi Dkt. Jacob Chimeledya, Mkuu wa Kanisa la Anglikan Tanzania, kuomboleza kifo cha Askofu Godfrey Mdimi Mhogolo wa Dayosisi ya Kati, Kanisa Anglikani, Dodoma kilichotokea tarehe 27 Machi, 2014 katika Hospitali ya Mil Park nchini Afrika Kusini alikokuwa amepelekwa kwa matibabu.

“Nimepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za kifo cha Mtumishi wa Mungu, Askofu Godfrey Mdimi Mhogolo aliyelitumikia Kanisa lake la Anglikana kwa uaminifu na uadilifu mkubwa, na ambaye mchango wake kwa maisha ya kiroho ya Waumini wake unajulikana kwa wengi miongoni mwetu”, amesema Rais Kikwete katika Salamu zake za Rambirambi.

Rais Kikwete amesema kuondoka kwa Askofu Mhogolo kumeacha pengo kubwa siyo tu kwa Waumini wa Kanisa la Anglikana katika Dayosisi yake, Dayosisi ya Kati, Dodoma bali pia kwa Waamini wote wengine wa Madhehebu hayo kote nchini, na kwa kweli wapenda amani wote popote walipo.

“Ni kutokana na msiba huu mkubwa, ninakutumia wewe Dkt. Jocob Chimeledya, Mkuu wa Kanisa la Anglikana Tanzania, na Waamini wote wa Kanisa hilo Salamu zangu za Rambirambi kutoka dhati ya moyo wangu kwa kuondokewa na Mtumishi huyu wa Mungu aliyejitoa kikamilifu kuwatumikia Waamini wa Kanisa lake”, ameongeza kusema Rais Kikwete na kuongeza, “Kupitia kwako naomba pia Salamu zangu za Rambirambi na Pole nyingi ziifikie familia ya Marehemu Askofu Godfrey Mdimi Mhogolo kwa kuondokewa na Kiongozi na mhimili wa familia yao”.

Rais Kikwete ameiomba familia ya Marehemu kuwa na moyo wa uvumilivu na subira katika kipindi hiki kigumu cha kuondokewa na Mpendwa wao kwa kutambua kuwa yote ni Mapenzi yake Mola.

“Ninaihakikishia familia ya Marehemu kuwa binafsi niko pamoja nao katika kuomboleza msiba huu mkubwa kwa kutambua kuwa msiba wao ni wetu sote. Namuomba Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema aipokee na kuilaza Mahala Pema Peponi, Roho ya Marehemu Askofu Godfrey Mdimi Mhogolo, Amina”, amemalizia kusema Rais Kikwete katika Salamu zake.








All the contents on this site are copyrighted ©.