Sakramenti ya Ekaristi Takatifu mintarafu mafundisho ya Mtakatifu Ambrosi
Padre Raniero Cantalamessa mhubiri wa nyumba ya Kipapa katika tafakari yake ya tatu
ya Kipindi cha Kwaresima kwa Baba Mtakatifu Francisko pamoja na wasaidizi wake wa
karibu, Ijumaa tarehe 28 Machi 2014, amezungumzia kuhusu Sakramenti ya Ekaristi Takatifu
mintarafu mafundisho ya Mtakatifu Ambrosi.
Baba huyu wa imani alifafanua vyema
kuhusu mageuzo kwa kusema kwamba, nguvu ya baraka yapita ile ya maumbile, kwani kwa
baraka maumbile yenyewe hujikuta yamebadilika. Neno la Kristo lililoweza kuumba kitu
kisichokuwapo bila kutumia kitu, lisingeweza kubadili vitu vilivyopo katika vile ambavyo
havikuwepo?
Katika tafakari yake, Padre Cantalamessa amezunguzia kuhusu Fumbo
la Ekaristi takatifu, Ekaristi Takatifu kama kielelezo na chemchemi ya baraka ya Agano
la Kale kati ya Mungu na Waisraeli. Ekaristi Takatifu ni sadaka na zawadi ya Kristo
kwa waja wake. Fumbo la Ekaristi takatifu linaunda Kanisa na kwamba, Ekaristi Takatifu
ni Kanisa lenyewe, kumbe wale wanaoshiriki Fumbo la Ekaristi Takatifu wanageuzwa na
kuwa ni sehemu ya Fumbo la Mwili wa Kristo yaani Kanisa.
Mtakatifu Ambrosi
anasema, Ekaristi Takatifu ni Fumbo la Mwili wa Yesu aliyezaliwa na Bikira Maria,
akateswa na kufa Msalabani na alipochomwa ubavuni kwa mkuki, ikatoka maji na damu.
Mwili wa Kristo unaweza kueleweka katika maana kuu tatu yaani: Mwili wa kweli wa Yesu
aliyezaliwa na Bikira Maria; Mwili wa Kristo, yaani Ekaristi Takatifu na Fumbo la
Mwili wa Kristo, yaani Kanisa.
Ekaristi Takatifu ni chimbuko la majadiliano
ya Kidini na Wayahudi, kwani kwa Wayahudi, Ekaristi inajulikana kama "Beraka" yaani:
Sala ya kubariki na kushukuru: kabla na baada ya chakula. Kwa Wakristo Ekaristi Takatifu
ni kielelezo cha Mwana Kondoo wa Pasaka na imepewa hadhi ya juu kabisa na Kristo mwenyewe,
kama kielelezo cha Agano Jipya na milele linalofungwa kwa Damu yake Azizi. Yesu anasema
Ekaristi ni Mwili na Damu yake inayomwagika kwa ajili ya wengi.
Yesu aliweka
Sakramenti ya Ekaristi Takatifu, siku ile iliyotangulia kuteswa kwake, yaani Ijumaa
kuu. Mazingira, Sala na vitendo vyote vinafanya rejea kwenye Karamu ya Wayahudi. Yesu
anatoa maana mpya ya Karamu hii kwa kuanzisha Agano Jipya na la Milele, kama kielelezo
cha sadaka ya wokovu kwa binadamu. Ekaristi Takatifu ni kumbu kumbu endelevu ya Sadaka
ya Kristo pale Msalabani.
Kwa mageuzo ya mkate na divai hufanyika mabadiliko
ya uwamo wote wa mkate katika uwamo wa Mwili wa Kristo na uwamo wote wa divai katika
uwamo wa Damu yake Azizi. Jambo la msingi ambalo linapaswa kuzingatiwa hapa ni imani
ya mwamini anayepokea Fumbo la Ekaristi Takatifu.
Yesu amejisadaka na kuwapatia
wafuasi wake zawadi kubwa ya Mwili na Damu yake Azizi, kama Sakramenti, mwaliko kwa
waamini kuwa kweli ni sadaka hai inayopendeza machoni pa Mwenyezi Mungu. Sadaka ya
Kristo ni kielelezo cha hali ya juu kabisa cha upendo kwa Baba yake wa mbinguni na
kwa mwanadamu na kwamba, mwanadamu anapaswa kujisadaka na anapokubali kwa kusema Amina,
anakubali kuwa ni sehemu ya Ekaristi: Fumbo la Mwili wa Kristo, Fumbo la Kanisa.
Padre
Cantalamesaa anasema, hapa Ekaristi Takatifu inaunda Kanisa, changamoto kwa waamini
wanaoshiriki Fumbo la Ekaristi Takatifu kuwa ni kielelezo cha upendo wa Mungu kwa
jirani zao, kwa kujisadaka na kuwasaidia katika hija ya maisha yao hapa duniani. Ni
mwaliko wa kudumisha umoja wa Kanisa la Kristo lililoenea sehemu mbali mbali za dunia
kwa kukiri uweza na utukufu wa Kristo.