Marehemu John Gabriel Tuppa, Mkuu wa Mkoa wa Mara, alikuwa ni kiongozi mpatanishi
na mwenye uwezo wa kuona mbali!
Mkoa wa Mara upo katika majonzi mazito kufuatia kifo cha ghafla cha Mkuu wake wa Mkoa
kilichotokea tarehe 25 Machi 2014 wilayani Tarime. Mheshimiwa John Gabriel Tuppa alikuwa
wilayani Tarime kwa shughuli ya kufunga mafunzo ya Mgambo katika kijiji cha Nyamwaga,
shughuli ambayo hakuifanya kufuatia kifo chake cha ghafla akingali katika ofisi ya
Mkuu wa Wilaya ya Tarime.
Tarehe 27 Machi 2014 imefanyika Misa Takatifu ya
kumwombea na kumuaga kabla ya mwili wake kusafirishwa kuelekea Kilosa, Mkoa wa Morogoro
kwa Mazishi. Misa hiyo ilifanyika katika Kanisa Kuu la Bikira Maria Mama wa Mungu
na iliongozwa na Mhashamu Askofu Michael Msonganzila wa Jimbo la Musoma. Misa hiyo
iliyofanyika kwa utulivu mkubwa ilihudhuriwa na mapadre wengi wa Jimbo la Musoma,
Watawa na viongozi wa madhehebu mbalimbali. Aidha ilihudhuriwa pia viongozi wengi
wa serikali na wa vyama mbalimbali vya siasa pamoja na umati mkubwa wa waamini na
wakazi wa mkoa wa Mara na mikoa ya jirani.
Katika salamu za rambirambi, Askofu
Michael Msonganzila alimtaja marehemu kuwa ni kiongozi mahiri na hodari katika kazi
ambaye mkoa na Taifa kwa ujumla limempoteza. “Katikati ya majonzi tuliyonayo, tunafarijika
kwa kuwa katika uhai wake, mpendwa wetu alimsadiki Kristo “ufufuo na uzima” (Yoh.
11:25). Tunamkabidhi kwake ampokee katika raha ya milele” aliongeza Askofu. Mahubiri
ya Askofu katika Misa hiyo yalijikita katika Somo la Injili iliyosomwa toka Mt. 5:1
– 12. Askofu alianza kwa kueleza kuwa injili hiyo inafundisha juu ya Maisha yenye
heri. “injili hii” aliongeza Askofu “pia ina majina mengi. Inaitwa Hotuba ya Yesu
Mlimani ili kutangaza rasmi ujumbe maalumu lakini pia inaitwa Katiba Mpya ya Yesu
aliyoitoa kwa ajili ya wanafunzi wake na wana wa Mungu wote”. Askofu aliendea kueleza
kuwa sote tunaalikwa kuishi maisha ya heri: kuwa maskini wa roho, yaani kutokuweka
mioyo yetu katika mali au madaraka; kuwa na huzuni, yaani kusikitika tunapoona mambo
yanayopingana na sheria za Mungu yanashamiri ilhali yale yanayoendana na sheria ya
Mungu yanadidimizwa; kuwa wapole, wenye huruma na wapenda haki.
“Katika jitihada
za kuuishi ukristo wake”, Askofu alibainisha “marehemu aliakisi heri ya kuwa wapatanishi.
Na katika utumishi wake amekuwa kiungo kizuri cha kupatanisha makundi mbalimbali”.
Katika kufafanua namna ambavyo marehemu ameiishi heri hii, Askofu hakusita kutaja
kuwa marehemu Mkuu wa Mkoa amekuwa mpatanishi kati ya viongozi wa dini, kati ya viongozi
wa vyama vya siasa na kati ya koo au jamii zilizokuwa zikihasimiana katika baadhi
ya maeneo ya wilaya ya Butiama, Tarime na kwingineko.
Aidha Askofu alimtaja
marehemu kuwa amekuwa mpatanishi kati ya binadamu na mazingira kwa kulinda mazingira
na uasili wake. Yeye alikuwa mstari wa mbele kupinga na kupambana na uvuvi haramu
ambao hauathiri tu mazalia na samaki kwa ujumla bali pia huathiri afya za watumiaji.
Tofauti
na wapatanishi wengine wengi, Askofu alibainisha kuwa marehemu hakuwa anasubiri mpaka
mambo yaharibike ndio aanze kupatanisha kwa kutuliza makundi yanayozozana. Yeye alijaliwa
kipaji cha kuona mbali na hivyo aliweza kuyaita makundi mbalimbali kujadili juu ya
hatari iliyo mbele. Hapo Askofu alitoa mwaliko kwa viongozi wetu kutambua kuwa wepesi
kutambua hatari zijazo na kuchukua hatua mapema.
Kabla ya kuhitimisha mahubiri
yake, Askofu alirejea katika wasifu wa marehemu uliosomwa mwanzoni mwa Misa. Alieleza
kuwa kati ya mengi yanayoonekana katika wasifu huo ni kwamba, marehemu aliandaliwa
kwa muda mrefu na kwa kufuata hatua mbalimbali. Aliandaliwa kielimu na aliandaliwa
kiutendaji kwa kushika nyadhifa mbalimbali katika maeneo mengi hapa nchini. Kwa maandalizi
hayo aliwataka wakazi wa mkoa wa Mara kujihisi wenye bahati kwa kuhudumiwa na mtu
kama huyo.
Mwisho aliwaalika viongozi wa serikali kutokuona haya kuyaendeleza
mazuri aliyofanya katika sekta mbalimbali hapa mkoani. Alimaliza kwa kuwahakikishia
sala na matashi yake mema kwa familia, ndugu, jamaa na wakazi wote wa Mara katika
kipindi hiki cha majonzi.
Marehemu John Gabriel Tuppa alizaliwa Kilosa tarehe
01. 01. 1950. Alianza utumishi serikalini mwaka 1976 katika sekta ya elimu na kisha
kuendelea katika idara mbalimbali. Tangu septemba 2011 hadi mauti yanamkuta alikuwa
Mkuu wa Mkoa wa Mara.
Raha ya Milele Umpe ee Bwana na Mwanga wa Milele Umwangazie,
Apumzike kwa Amani. Amina.
Taarifa hii imeandaliwa na Padre William Bahitwa,
Jimbo Katoliki Musoma.