Dhamana ya Familia katika utunzaji bora wa mazingira katika Jamii ndiyo kauli mbiu
inayoongoza warsha ya siku moja iliyoandaliwa na Baraza la Kipapa la Familia kwa kushirikiana
na Greenaccord itakayofanyika tarehe 29 Machi 2014. Kanisa linatambua dhamana na wajibu
wa familia katika kulinda na kutunza mazingira ambayo ni sehemu ya kazi ya uumbaji.
Lengo la warsha hii ni kuibua mbinu mkakati utakaosaidia kuchangia mawazo
kwa ajili ya Maadhimisho ya Sinodi maalum ya Maaskofu kwa ajili ya Familia, itakayoadhimishwa
mjini Vatican, kuanzia tarehe 5 hadi tarehe 19 Oktoba, 2014. Familia zinapaswa kusaidiwa
kujenga utamaduni wa kulinda na kuhifadhi mazingira. Hii ndiyo changamoto kubwa iliyoko
mbele ya Jumuiya ya Kimataifa kadiri ya ushauri kutoka kwa wataalam wa masuala ya
mazingira.
Mada hii ni changamoto kwa washiriki kufanya rejea katika hati
na nyaraka mbali mbali zilizowahi kutolewa na Mama Kanisa kuhusiana na mazingira,
mwaliko na changamoto ya kubadili mfumo wa maisha, unaowajibisha familia.Familia hazina
budi kuchangia katika mchakato wa ujenzi wa Jamii inayojikita katika utunzaji bora
wa mazingira.
Askofu mkuu Vincenzo Paglia atakuwa ni kati ya wawezeshaji wakuu
kwenye warsha hii ya siku moja itakayofanyika mjini Vatican pamoja na kuwahusisha
viongozi wakuu wa kidini, wachumi, watafiti na wadau mbali mbali wa mazingira.