Kama ilivyokuwa kwa Manabii, wito wa Yesu wa toba na wongofu wa ndani haulengi kwanza
kazi za nje yaani kuvaa gunia na kujipaka majivu, kufunga na kujitesa, bali wongofu
wa moyo unaogusa undani wa mtu mzima. Bila wongofu huu, matendo ya toba hayana nguvu
wala ukweli ndani yake. Wongofu wa ndani husukumwa kuonesha ishara zinazoonekana,
vitendo vya mwili, na kazi za toba.
Toba ya ndani
ni kuelekeza upya kabisa maisha yote, ni kurudi na kumwongokea Mwenyezi Mungu kwa
moyo wote, kukataa dhambi na nafasi zake; kuchukua maovu, kwa kujiwekea lengo ka kubadili
maisha pamoja na kuendelea kutumainia huruma na neema ya Mungu. Wongofu wa ndani hufumbata
maumivu na machungu ya wokovu ambayo Mababa wa Kanisa wameita kuwa ni taabu ya roho
au toba ya moyo.
Moyo wa mtu ni mzito na mgumu. Inatakiwa Mwenyezi Mungu ampe
mtu moyo mpya. Ikumbukwe kwamba, wongofu wa ndani ni kazi ya neema ya Mungu inayoufanya
moyo wa mwanadamu uweze kumrudia tena Muumba wake, kwa kugundua ukuu, huruma na mapendo
ya Mungu yasiyokuwa na kifani. Mwamini anapaswa kuonesha masikitiko ya dhambi zake,
kwa kumwangalia Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka ili kumkomboa mwanadamu kutoka
katika lindi la dhambi na mauti. Kwa Damu yake azizi, Yesu amemkomboa mwanadamu na
kuukirimia ulimwengu neema ya toba na wongofu wa ndani.
Mama Kanisa amewawekea
watoto wake nyakati za toba zinazojikita katika mazoezi ya maisha ya kiroho, liturujia,
hija, kujinyima, kufunga na kusali pamoja na kushiriki katika kazi za matendo ya huruma
na kimissionari. Kwa kutambua umuhimu wat oba na wongofu wa ndani, Baba Mtakatifu
Francisko, ametenga Ijumaa ya tarehe 28 Machi 2014 kuwa ni siku maalum ya toba na
wongofu wa ndani, mwaliko wa kuchuchumilia Sakramenti ya Upatanisho, inayomwonjesha
mwamini huruma na upendo wa Mungu usiokuwa na kifani.
Hii ni mikakati ya shughuli
za kichungaji inayotekelezwa na Baraza la Kipapa la Uinjilishaji Mpya. Baba Mtakatifu
Ijumaa, majira ya jioni ataongoza Ibada ya Upatanisho kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu
Petro mjini Vatican na baadaye atapata fursa ya kuungamisha baadhi ya waamini watakaoshiriki
katika Ibada hii na baadaye kutoa ondoleo la dhambi.
Kuanzia majira ya Saa
mbili kamili asubuhi, Kanisa la Mtakatifu Agnes, Bikira Maria, Trastevere na Kanisa
la Madonda Matakatifu, yataendelea kutumika kwa ajili ya Ibada ya Kuabudu Ekaristi
Takatifu kwa muda wa Masaa 24. Hayo yamesemwa na Askofu mkuu Rino Fisichella, Rais
wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji Mpya. Ni tukio ambalo litawahusisha vijana ambao
kimsingi ni Wainjilishaji wapya kwa kuwakaribisha vijana wenzao, kuingia ndani ya
Kanisa, ili kuonja huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake. Ndani ya Makanisa haya,
watakutana na Mapadre ambao watakuwa tayari kuzungumza nao na hatimaye, kuwaungamisha.
Tukio hili la kihistoria, anasema, Askofu mkuu Fisichella, litahitimishwa
kwa Ibada ya Masifu ya kwanza ya Jioni, Jumapili ya Nne ya Kipindi cha Kwaresima,
Ibada itakayofanyika kwenye Kanisa la Santo Spirito in Sassia, Jimbo kuu la Roma.