2014-03-27 09:45:34

Sikilizeni sauti ya Mungu, msielemewe na ubinafsi, rushwa na ufisadi!


Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi, tarehe 27 Machi 2014 ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro, na kuhudhuriwa na wabunge 493 wa Bunge la Italia. Katika mahubiri yake, Baba Mtakatifu amewakumbusha wabunge hao kwamba, nyakati za Yesu kulikuwepo na viongozi ambao walielemewa sana na ubinafsi, uchu wa mali na madaraka, kiasi cha kuendekeza kinzani na migogoro ya kijamii, hata pale Yesu Kristo Masiha alipokuja wakashindwa kumtambua na badala yake wakamtuhumu kwamba alikuwa na mdau wa Shetani.

Somo la kwanza anasema Baba Mtakatifu linaonesha masikitiko na lawama inayotolewa na Nabii Yeremia kwa Waisraeli ambao hawakusikiliza sauti ya Mungu na kuenenda katika njia zake, kiasi kwamba, walishindwa kupata maendeleo. Ni watu walioshindwa kuwapokea Manabii waliotumwa na Mungu kwa kufanya shingo yao kuwa ngumu pamoja na kuwatenda jeuri. Baba Mtakatifu anasema, hiki ni kilio cha Mwenyezi Mungu kinachojionesha hata katika Injili ya Leo, kwani watu walishindwa kusikia sauti ya Mungu.

Kutokana na kuelemewa mno na dhambi pamoja na ubinafsi wao, wakajikuta wanatumbikia katika rushwa na ubadhirifu wa mali ya umma, hata hivyo bado Mwenyezi Mungu aliendelea kuwasubiri ili aweze kuwaonjesha huruma na upendo wake usiokuwa na kifani. Ushuhuda wa maisha ya Yesu uliojikita katika huduma, huruma na mapendo, uliwachefua viongozi wa Wayahudi kiasi kwamba, wakaanza kufanya njama ya kutaka kumwangamiza.

Viongozi hawa walikosea na kupoteza dira na mwelekeo wa maisha yao; wakatindikiwa katika imani kiasi cha kushindwa kuupokea wokovu na upendo uliokuwa unatangazwa na Yesu; wakagubikwa katika ubinafsi badala ya kujiachilia huru mbele ya Yesu. Baba Mtakatifu anasema, Mwenyezi Mungu ni mwingi wa huruma na mapendo. Watu wanajiangaisha mno kwa maisha ili waweze kuonekana kuwa wema, lakini ndani mwao wanaficha tabia chafu, ni wanafiki sawa na makaburi yaliyopakwa chokaa.

Baba Mtakatifu Francisko anahtimisha mahubiri yake kwa kusema kwamba, Kipindi cha Kwaresima, kinamwezesha mwamini kuonja tena huruma na upendo wa Mungu, changamoto na mwaliko kwa mwamini kujiweka wazi mbele ya Mungu, kwa kutembea katika njia ya haki na wokovu unaotoka kwa Mungu mwenyewe. Baba Mtakatifu anawataka waamini kuwa thabiti katika imani na wala si kama walivyofanya wakuu wa makuhani walioyakita maisha yao katika imani potofu, kiasi cha kuwaongoza watu katika njia mbaya!







All the contents on this site are copyrighted ©.