Yerusalemu ni kisima cha imani na mahali ambapo mwamini anapata nafasi ya kutembea
na kukutana na Yesu katika hja ya maisha yake ya hapa duniani, tayari kushiriki katika
mchakato wa kujitakasa kwa kugusa maeneo matakatifu. Ni fursa ya kuweza kuyafahamu
zaidi Maandiko Matakatifu, tayari kuganga na kuponya utupu wa ndani, kwa kufunikwa
na kivuli cha uwepo wa Kristo mwenyewe katika maeneo haya matakatifu.
Ni mwaliko
wa kushiriki katika toba na wongofu wa ndani, kwa kugusa maeneo ambayo yalitumiwa
na Yesu mwenyewe katika maisha yake ya hadhara hapa duniani na hatimaye, akajisadaka
pale Mlimani Kalvari kwa ajili ya kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi
na mauti.
Ni tafakari ya kina inayotolewa na Kardinali Leonardo Sandri, Mwenyekiti
wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya Makanisa ya Mashariki, wakati huu Mama Kanisa anapoendelea
kuwaandaa waamini na watu wote wenye mapenzi mema hija ya kitume ya Baba Mtakatifu
Francisko huko katika Nchi Takatifu. Kaburi takatifu ni kiini cha imani ya Kikristo
kwani linamwonesha Kristo aliyeteswa, akafa, akazikwa na kufufuka. Mji wa Bethelehemu
ni mahali ambapo binadamu alitangaziwa ujumbe wa amani kwa kuzaliwa kwa Mwana wa Mungu.
Ziwa Galilaya ni mahali penye umaarufu wa pekee kwani hapa Yesu alituliza
dhoruma lililokuwa linawayumbisha mitume kiasi cha kuanza kuchungulia kifo, ni mahali
ambapo hata leo hii, Yesu anaendelea kutuliza dhoruba katika maisha na utume wa Kanisa.
Kapernaumu ni mahali ambapo Yesu alitoa muhtasari wa mafundisho yake makuu yanayofumbatwa
katika Heri za Mlimani. Mjini Yerusalemu, Kanisa linakumbuka Siku ile Yesu alipoweka
Sakramenti ya Ekaristi Takatifu na Daraja Takatifu, akawaonesha mitume wake upendo
unaojikita katika huduma. Hii ni changamoto kwa waamini wote ndani ya Kanisa.
Yerusalemu
ni mji ambamo, Mitume walisali pamoja na Bikira Maria hadi pale Roho Mtakatifu alipowashukia,
wakatoka vifua mbele kuwatangazia watu wa mataifa, Injili ya Furaha inayobubujika
kutoka kwa Yesu Kristo aliyeteswa, akafa na kufufuka kutoka katika wafu! Kumbe, hija
katika Nchi Takatifu inasheheni utajiri mkubwa wa maisha ya kiroho, ndiyo maana Mama
Kanisa anawachangamotisha watoto wake na watu wote wenye mapenzi mema, kumsindikiza
Baba Mtakatifu Francisko kwa njia ya sala na sadaka zao wakati wa hija yake ya kitume
katika Nchi Takatifu.
Kardinali Sandri anasema, hija hii pamoja na mambo mengine,
inalenga kukoleza moyo na mchakato wa majadiliano ya amani yanayosimikwa katika ukweli,
uwazi, kuheshimiana na kuthaminiana, ili kudumisha misingi ya haki, amani, upendo,
udugu na mshikamano wa kweli. Ni mwaliko wa kujenga na kudumisha moyo wa upatanisho
wa kitaifa, ili kuvuka vikwazo vya woga na wasi wasi na hatimaye, amani na utulivu
viweze kutawala tena katika maisha ya wananchi.
Baba Mtakatifu katika hija
yake ya kitume, atatembelea Amman, mahali ambako kuna kundi kubwa la wakimbizi na
wahamiaji wanaoteseka kutokana na vita inayozidi kupamba moto huko Mashariki ya Kati.
Hapa Baba Mtakatifu anapenda kuwaonjesha wote hao upendo na mshikamano kutoka kwa
Mama Kanisa kwa maskini na wote wanaokabiliwa na majanga ya maisha.
Ikumbukwe
kwamba, hii ni hija ya kitume inayosimikwa katika kukoleza majadiliano ya kiekumene
miongoni mwa Wakristo, kwa kufanya kumbu kumbu ya Jubilee ya Miaka 50 tangu Papa Paulo
sita alipokutana, akasali na kuzungumza na Patriaki Anathegoras wa Yerusalemu, miaka
hamsini iliyopita. Tukio hili linatarajiwa kufanya kwenye Kaburi Takatifu, mahali
ambapo pia pamekuwa ni kielelezo cha utengano kati ya Wakristo. Ndiyo maana kauli
mbiu ya Hija hii ya Kitume ina mwelekeo wa Kiekumene, ili wote wawe wamoja!
Kardinali
Sandri aliyebahatika kufanya kazi karibu sana na Mwenyeheri Yohane Paulo II anasema,
kati ya kumbu kumbu ambazo zimebaki moyoni na akilini mwake, ni pale alipokwenda kumtembelea
Mwenyeheri Yohane Paulo II alipokuwa amelazwa kwa mara ya pili Hospitalini Gemelli.
Alimwona akiwa katika mateso na mahangaiko ya ndani, akamwambia, naomba mnirudishe
nyumbani, niko tayari kuungana na Yesu Kristo aliyeteseka, akafa na kufufuka kwa ajili
yetu! Mwenyeheri Yohane Paulo II alionesha ujasiri wa ajabu kiasi cha kuwashangaza
wale waliokuwepo chumbani humo.