Majadiliano ya kidini yapate chimbuko lake katika uhalisia wa maisha ya watu!
Kardinali Orlando Beltran Quevedo, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Mindanao, lililoko
Kusini mwa nchi ya Ufilippini anasema, ataendelea kujielekeza zaidi na zaidi katika
mchakato wa majadiliano ya kidini kama njia ya kujenga na kudumisha misingi ya haki,
amani na upatanisho wa kitaifa.
Kwa miaka
mingi Kardinali Quevedo amekuwa akijihusisha na mchakato wa majadiliano ya kidini
na amani kati ya Wakristo na Waislam, Kusini mwa Ufilippini. Hivi karibuni alipokuwa
anazungumza na Jumuiya ya Wafilippini mjini Roma alisema kwamba, mpasuko na kinzani
kati ya Wakristo na Waislam nchini Ufilippini ni matokeo ya watu kutoaminiana ndani
ya Jamii na baadhi ya watu kuendekeza habari za uzushi zisizo na mafao wala mashiko
kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wananchi wa Ufilippini: kiroho na kimwili.
Kardinali
Quevedo anasema, majadiliano ya kidini kati ya Waislam na Wakristo hayana budi kujikita
katika ngazi kuu tatu: yaani: majadiliano ya maisha; majadiliano yanayoshirikisha
mang’amuzi na uzoefu wa maisha ya kiroho pamoja na majadiliano yanayojikita katika
taalimungu; majadiliano ambayo yanawahusisha wataalam wa masuala kitaalimungu kutoka
katika dini hizi mbili.
Majadiliano yanayojikita katika maisha yanawajengea
uwezo waamini wa dini hizi mbili kuheshimiana, kuthaminiana na kusaidiana kwa hali
na mali, licha ya tofauti zao za kidini, kwani wote wameumbwa kwa sura na mfano wa
Mungu. Majadiliano haya yaanzie katika shule na taasisi za malezi kwa watoto na vijana
wa kizazi kipya kwa kutambua kwamba, hawa ndio tumaini na jeuri ya taifa. Ni watoto
wanaoweza kusoma na kuishi pamoja kwa amani na utulivu kabisa bila ya chokochoko zozote.
Kardinali
Quevedo anasema, majadiliano yanayojikita katika mang’amuzi ya maisha ya kiroho yanalenga
kushirikishana tunu msingi za maisha ya kidini zinazofumbatwa katika haki, amani,
upendo na mshikamano. Juhudi hizi zinaonekana hasa katika huduma kwa maskini na wote
wanaosukimizwa pembezoni mwa Jamii. Hizi ni huduma zinazofanywa na taasisi mbali mbali
za dini ya Waislam na Wakristo bila upendeleo, lakini wakisukumwa zaidi na upendo
kwa Mungu na jirani.
Majadiliano katika misingi ya kitaalimungu inawapatia
waamini wa dini hizi mbili kufahamu mafundisho tanzu ya dini hizi kama yanavyofafanuliwa
na wataalam wa taalimungu. Kuna mada zinazofanana katika Kitabu Kitukufu cha Koran
na Biblia: Kwa mfano: kazi ya uumbaji na utunzaji bora wa mazingira; athari za mabadiliko
ya tabianchi pamoja na maisha ambayo ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Hizi
ni tema zinazoweza kufafanuliwa vyema na wataalam wa dini hizi mbili.
Kardinali
Quevedo anasema, wengi wanaona kuteuliwa kwake na Baba Mtakatifu Francisko kuwa Kardinali
ni kitendawili, ambacho anasema, angependa kukitegua. Tangu mwaka 1974, amekuwa mstari
wa mbele katika kuibua, kupanga na kutekekeza mikakati ya shughuli za kichungaji kwa
Kanisa Barani Asia. Ametamani kuona Kanisa ambalo liko kati ya watu kwa ajili ya kuwahudumia
watu katika mahitaji yao msingi: kiroho na kimwili. Kutokana na mchango wake katika
maisha na utume wa Kanisa amewahi kuwa ni kati ya Maaskofu waliopigiwa kura nyingi
kwenye Maadhimisho ya Sinodi za Maaskofu.
Mwishoni Kardinali Orlando Beltran
Quevedo wa Jimbo kuu la Mindanao anasema kwamba, yeye amesomea na kufaulu kupata shahada
ya uzamivu katika masuala ya elimu. Haikuwa rahisi kwake, kwani alipokuwa anakaribia
kuhitimisha kuandika kazi yake, Mkuu wake wa Shirika alimtaka kurudi haraka Shirikani
kwani alikuwa anahitajika kuwa ni Rais wa Chuo Kikuu cha Notre Dame, hapo utii ukashinda
kiburi na matamanio ya kibinadamu. Kwa hakika hapa Waswahili wangelisema, “Usione
vinaelea, ujue kwamba, vieumbwa”!