Chama cha Legio Maria chatambuliwa rasmi na Kanisa
Baraza la Kipapa la Walei, Alhamisi tarehe 27 Machi 2014 limekabidhi hati ya utambulisho
kwa Chama cha Kitume cha Legio Maria kuonesha kwamba kwa sasa kinatambuliwa rasmi
ndani ya Kanisa Katoliki. Hati hii imetolewa na Askofu mkuu Joseph Clemens, Katibu
mkuu wa Baraza la Kipapa la Walei katika hafla ambayo imehudhuriwa na viongozi wa
Kanisa na wakuu wa Chama cha Legio Maria.
Chama cha Legio Maria kilianzishwa
kunako mwaka 1921 huko Dublin, Ireland na Kikundi cha waamini kilichokuwa chini ya
uongozi na usimamizi wa Bwana Franck Duff, mfanyakazi katika Wizara ya fedha na baadaye
akawa ni Katibu muhtasi wa Waziri wa Ulinzi nchini Ireland. Chama hiki kimedumu takribani
miaka 93 bila ya kutambuliwa rasmi na Kanisa. Lakini katika kipindi chote hiki, Chama
kimeendelea kuwafunda waamini na hatimaye kikaanza kuwa na utambulisho wake maalum
ndani ya Kanisa.
Chama cha Legio Maria kinachota utajiri wake kutoka katika
tasaufi ya Bikira Maria pamoja na kujiaminisha kwa nguvu ya Roho Mtakatifu, anayewahamasisha
wanachama wa Legio Maria kuwa na malengo makini sanjari na kuchuchumilia utakatifu
wa mtu binafsi, pamoja na kuendelea kushiriki kikamilifu katika mchakato wa Uinjilishaji
Mpya na huduma makini kwa maskini na wanyonge, bila kuwasahau wale waliokengeuka katika
imani yao kwa Kristo na Kanisa lake.
Askofu mkuu Joseph Clemens katika hotuba
yake wakati wa kukabidhi Haki na katiba ya Chama cha Legio Maria anasema, chama hiki
kimekuwa ni alama wazi kutoka kwa Roho Mtakatifu inayoonesha ari na moyo wa kimissionari
kati ya waamini walei, wanavyojitahidi kuyatakatifuza malimwengu kwa njia ya maisha
ya kawaida katika familia na sehemu mbali mbali za Kazi. Wanachama wa Legio Maria
wanajitahidi kumwilisha katika uhalisia wa maisha ule wito wa kuchuchumilia utakatifu
waliopewa wakati wa kupokea Sakramenti ya Ubatizo.