2014-03-26 07:29:10

Papa Francisko ni mjumbe wa matumaini, amani na upatanisho kwa Bara la Asia!


Hija ya kichungaji inayotarajiwa kufanywa na Baba Mtakatifu Francisko, Korea ya Kusini, kama sehemu ya Maadhimisho ya Siku ya Sita ya Vijana Barani Asia, ni tukio muhimu sana si tu kwa ajili ya Korea ya Kusini, bali kwa Bara zima la Asia. Hii ni kutokana na ukweli kwamba, Baba Mtakatifu Francisko anaifanya hija hii ya kitume kama mjumbe wa amani, mwenye uwezo wa kuzima kiu na matamanio ya watu wanaotaka kuona amani na utulivu; umoja na mshikamano wa kidugu vikatawala kati ya watu.

Ni maneno ya Askofu Peter Kang U-il, Rais wa Baraza la Maaskofu Korea, wakati huu Kanisa nchini humo linapojiandaa kwa hija ya kichungaji ya Baba Mtakatifu itakayofanyika kuanzia tarehe 14 hadi tarehe 18, Agosti, 2014. Kanisa lina matumaini makubwa kwamba, hija hii ya kichungaji itasaidia kuleta mwamko na ari kubwa zaidi katika mchakato wa Uinjilishaji Mpya nchini Korea na kwamba, waamini wataweza kutoka kifua mbele ili kushuhudia imani yao kwa Kristo na Kanisa lake.

Wananchi wa Korea katika ujumla wao, wanahamu kubwa ya kumwona na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko, kumbe uwepo wake ni kielelezo tosha kabisa cha matumaini ya wananchi wa Korea na Asia katika ujumla wake. Wananchi wanamsubiri kwa vile ni mjumbe wa amani, haki na upendo, hasa kwa wale wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii. Wananchi wa Korea wangependa kuona umoja na mshikamano wa kitaifa kati ya Korea ya Kaskazini na Korea ya Kusini; nchi mbili pacha ambazo zimekuwa zikisigana kwa takribani miaka 60 kwa sasa.

Baba Mtakatifu katika "Mkoba wake" hataacha kuchukua ujumbe wa upatanisho kati ya Nchi hizi mbili; ujumbe wa upatanisho, haki na amani huko Japan na China. Wananchi wanaendelea kujiandaa kikamilifu kwa hija ya kichungaji ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Korea ya Kusini.

Kauli mbiu inayoongoza Maadhimisho ya Siku ya Sita ya Vijana wa Barani Asia kwa Mwaka 2014 ni "Vijana wa Asia amkeni, utukufu wa mashahidi utawang'aria". Tukio hili linatarajiwa kukusanya vijana kutoka katika nchi 29 za Kiasia. Akiwa nchini Korea ya Kusini, Baba Mtakatifu Francisko anatarajiwa kuwatangaza watumishi wa Mungu 124 kutoka Korea, kuwa ni Wenyeheri.







All the contents on this site are copyrighted ©.