2014-03-26 12:03:44

Misimamo mikali ya kidini ni sumu ya amani na utulivu!


Hali ya wananchi kutoka Jamhuri ya Afrika ya Kati bado ni tete kwani wengi wao bado wanaendelea kushambuliwa, wanaishi katika kambi za wakimbizi na watu wasiokuwa na makazi; usalama na amani bado haujrejea katika hali yake ya kawaida; umaskini, njaa na maradhi, bado yanawaandama wananchi wengi. Haya ni kati ya mambo mazito ambayo Askofu mkuu Dieudonnè Nzapalainga wa Jimbo kuu la Bangui alikuwa amebeba moyoni mwake, wakati wa Katekesi ya Baba Mtakatifu Francisko, mjini Vatican siku ya Jumatano, tarehe 26 Machi 2014.

Wananchi wanataka kuona amani, usalama na utulivu vinarejea tena, lakini kwa bahati mbaya Seleka na Balaka bado wanaendelea kusababisha hofu na wasi wasi mkubwa nchini humo. Wananchi wanaiomba Jumuiya ya Kimataifa kusaidia mchakato wa kurejesha amani na utulivu nchini Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati. Haiwezekani kwamba, Jumuiya ya Kimataifa inafumbia macho mateso na mahangaiko ya wananchi wa Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati, kwani wana wajibika kimaadili!.

Kwa upande wake Imam Oumar Kobine Layama wa mji wa Bangui anasema, kuna haja kwa Serikali na watu wake kulinda na kudumisha uhuru wa kidini, kwa kuheshimiana na kuthaminiana kwa kutambua kwamba, wote ni watoto wa Mungu mmoja na kamwe imani isiwe ni sababu na chanzo cha uvunjifu wa amani na utulivu. Misimamo mikali ya kidini na kiimani ni sumu ya amani, utulivu na maendeleo ya watu. Waamini wa dini mbali mbali wajenge utamaduni wa kuvumiliana na kusaidiana, kwani hizi ni tunu msingi za maisha ya kiroho kwa kila mwamini.

Umoja na mshikamano wa kitaifa; amani na utulivu; mafao na ustawi wa wengi anasema Imam Oumar Kobine Layama kuwa ni mambo msingi katika kuvuka vishawishi vya kinzani na utengano kati ya watu. Kila upande unapaswa kuchukua dhamana kwa kuchunguza kutoka katika undani wao, jinsi ambavyo kama waamini wamechangia kubomoka kwa msingi wa haki, amani na utulvu nchini humo. Imani thabiti, iwe ni msingi wa ujenzi wa haki na amani kati ya watu! Wananchi kutoka Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati wanapaswa sasa kuanza mchakato wa haki, amani, upatanisho na mshikamano wa kitaifa, wakisaidiwa na Jumuiya ya Kimataifa!







All the contents on this site are copyrighted ©.