Kiburi cha mwanadamu ni kaburi la maisha yake ya kiroho!
Kwaresima ni kipindi cha toba na wongofu wa ndani; ni kipindi cha kusali na kufunga
ni wakati muafaka uliokubalika wa kumwilisha imani katika matendo kwa njia ya huduma
ya upendo kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii. Wongofu wa ndani
ni mchakato wa kuikimbia dhambi na nafasi zake, jambo ambalo limehubiriwa na Mama
Kanisa kwa kitambo kikubwa.
Kufunga na
kusali ni kitendo cha kukimbilia huruma ya Mungu kwa ajili ya maondoleo ya dhambi,
ili kuganga madonda ya dhambi yanayoendelea kumwandama mwamini katika hija ya maisha
yake hapa duniani. Kufunga na kusali kunapania kuimarisha utashi na malengo ya mwamini
katika kuchuchumilia utakatifu wa maisha kwa kuondokana na na kiburi ambalo limekuwa
ni kaburi la maisha ya kiroho.
Hizi ndizo changamoto zinazotolewa na Patriaki
Fouad Twal wa Yerusalemu katika ujumbe wake wa Kwaresima kwa Mwaka 2014. Anasema,
upendo kwa jirani wanaoteseka kutokana na hali mbali mbali za maisha, hauna budi kuwa
ni kielelezo cha umwilishaji wa Injili katika huduma na matendo adili. Huduma hii
inapaswa pia kujikita katika mchakato wa upatanisho kati ya Mungu na jirani na kati
ya mtu na mtu pamoja na kuonesha jitihada za kupokea huruma na upendo wa Mungu kwa
njia ya Sakramenti ya Upatanisho.
Patriaki Twal anasema, sadaka iwe ni kile
ambacho mtu katika undani wa maisha yake anakipenda na anapokitoa kinagusa undani
wake. Hii ndiyo maana ya matendo ya huruma yanayotekelezwa na waamini katika kipindi
hiki cha Kwaresima, kama alivyofanya yule mwanamke mjane aliyetoa hadi senti yake
ya mwisho. Sala ni kati ya mambo msingi yanayotiliwa mkazo na Mama Kanisa katika
kipindi hiki cha Kwaresima kwani ni daraja kati ya kufunga na kutoa sadaka. Huu ni
mwaliko kwa waamini kuhakikisha kwamba, wanashiriki katika adhimisho la Fumbo la Ekaristi
Takatifu, kila Jumapili.
Familia zijenge na kuimarisha utamaduni wa kusali
pamoja katika hali ya utulivu bila kuingiliwa na milio ya simu, televisheni au radio,
ili kuwawezesha wanafamilia kuindia katika undani wa maisha yao ili wapate kukutana
na Yes una hatimaye kumkaribisha ili aweze kuibariki familia inayokutana katika sala.
Patriaki
Fouad Twal wa Yerusalemu anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kujitokeza
kwa wingi katika maadhimisho ya Jumapili ya Matawi, Kanisa linapofanya kumbu kumbu
endelevu ya Siku ile Yesu alipoingia Yerusalemu kwa shangwe, huku Watoto wa Wayahudi
wakitandaza nguo zao njiani, kuonesha ukuu na utukufu wa Yesu Kristo, Masiha na Mkombozi
wa dunia. Maandamano ya Jumapili ya Matawi yataanzia kwenye Mlima wa Mizeituni, tayari
kuelekea mjini Yerusalemu, ili kushiriki kikamilifu katika Fumbo la Pasaka, yaani:
mateso, kifo na ufufuko wa Yesu.
Waamini wanaweza kuboresha hija ya maisha
yao wakati huu wa Kwaresima kwa kutembelea na kuangalia Onesho la Picha za Papa Paulo
VI alipotembelea Nchi Takatifu yapata miaka hamsini iliyopita.
Ujumbe huu umehaririwa
na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.