Askofu mkuu Josephat Louis Lebulu wa Jimbo kuu la Arusha Tanzania, katika mahojiano
maalum na Radio Vatican kuhusu maisha na wito wa Kipadre, wakati huu Baba Mtakatifu
Francisko anapotafakari kuhusu Sakramenti ya Daraja Takatifu. Anasema, katika maisha
yake, alitamani sana kuwa na elimu bora ya yenye kiwango cha juu, hamu ambayo inapaswa
kuratibiwa miongoni mwa Majandokasisi.
Alibahatika
kuona mifano ya Mapadre wema, watakatifu na wachapakazi hodari, waliomsaidia katika
majiundo yake katika maisha na wito wa Kipadre bila kusahau maadhimisho ya Mafumbo
mbali mbali ya Kanisa kwa ajili ya kumtukuza Mwenyezi Mungu na mwanadamu kutakatifuzwa.
Anasema, Mapadre wanapaswa kuwa na msimamo thabiti katika maisha yao na kwamba, katika
hija ya maisha yake ya Kipadre amebahatika pia kukutana na kufanya kazi na waamini
walei, waliomsaidia na kumsindikiza katika sala na sadaka zao.
Askofu mkuu
Lebulu anasema, furaha ya Upadre ni kuishi na wengine katika Jumuiya, kushikamana
katika utume, kwani maisha ya Padre mpweke, yanaweza kumtumbukiza katika majanga na
hatimaye, akamezwa na malimwengu. Maisha na wito wa Kipadre unakuwa na kuboreka kwa
kujenga na kuimarisha mahusiano thabiti na wengine; kwa njia ya sala na tafakari ya
Neno la Mungi; kwa kuwa na msimamo thabiti katika maisha, bila kuyumbishwa yumbishwa
kama "Daladala" iliyokatika usukani! Kamwe katika maisha yake hajawahi kujuta kwa
nini aliamua kuwa Padre!