2014-03-24 14:17:13

Wokovu unasimikwa katika fadhila ya unyenyekevu na imani thabiti!


Haitoshi kwa mwamini kushika Amri za Mungu,bali pia anapaswa kuwa na imani thabiti inayojikita katika unyenyekevu, ili kuonja huruma na upendo wa Mungu unaojionesha kwa watu wake bila ubaguzi. Katika Agano la Kale, mtu mwenye ugonjwa wa Ukoma alikuwa anatengwa na jamii na kwamba, wajane waliteseka sana katika Jamii kutokana na mfumo dume! Yesu anasema kwamba, wote hawa wanahitaji kushirikishwa katika kazi ya ukombozi.

Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri yake siku ya Jumatatu, tarehe 24 Machi 2014 kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha, kilichoko mjini Vatican anasema, kwamba, Yesu kwa kumponya mkoma, anachafua hali ya hewa kiasi kwamba, Wakuu wa Makuhani wanaanza kutunga njama ya kumuua Yesu. Unyenyekevu wa moyo na upole, ulimwezesha Naamani mtu wa Shamu kuponyeshwa Ukoma wake na Nabii Elisha.

Baba Mtakatifu anawaambia waamini kwamba, ikiwa kama wanataka kukombolewa na Yesu, hawana budi kujikita katika unyenyekevu, ili kuonja huruma na upendo wake hata katika dhambi na mapungufu ya kibinadamu. Fadhila ya unyenyekevu, iwawezesha waamini kusimamia ukweli kwa kutambua udhaifu wao, tayari kukimbilia huruma na upendo wa Mungu kwa njia ya Sakramenti ya Upatanisho.







All the contents on this site are copyrighted ©.