Upendo na huruma ya Mungu ina nguvu ya kuvuka mawazo mabaya!
Liturujia ya Neno la Mungu, Jumapili ya tatu ya Kipindi cha Kwaresma inamwonesha Yesu
akizungumza na mwanamke Msamaria, mazungumzo ambayo yalisaidia kuvunjilia mbali uhasama
na chuki iliyokuwepo kati ya Wayahudi na Wasamaria, kiasi hata cha kuweza kupenya
katika undani wa maisha ya mwanamke Msamaria. Yesu anafanya yote haya bila wasi wasi
wala woga, anakutana na mwanamke ambaye anapenda kumwonjesha upendo wa dhati, unaoleta
mabadiliko ya ndani kwa kuvuka mawazo mabaya kwa kukumbatia uhalisia wa maisha!
Ni
sehemu ya tafakari iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, wakati wa Sala ya Malaika
wa Bwana, kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro, uliokuwa umefurika kwa mahujaji
kutoka sehemu mbali mbali za dunia, Jumapili tarehe 23 Machi 2014. Yesu alimwomba
mwanamke Msamaria maji ya kunywa ili kuamsha ndani mwake ile kiu ya kutaka kukutana
na Mwenyezi Mungu.
Hii ndiyo kiu ambayo iko katika maisha ya mwanadamu, lakini
kwa bahati mbaya, watu wengi bado hawajapata ujasiri wa kujadiliana na Yesu, kwa kuangalia
undani wa maisha yao, anasema Baba Mtakatifu Francisko! Mwanamke Msamaria ni changamoto
kwa waamini kuchunguza dhamiri zao ili hatimaye, kuwa na ujasiri wa kumwomba Yesu
maji yatakayozima kiu ya maisha ya uzima wa milele!
Mitume wa Yesu waliporejea
kutoka mjini, walishangaa kumwona Yesu akizungumza na Mwanamke Msamaria, lakini Baba
Mtakatifu anasema, huruma na upendo wa Mungu ni mkuu unashinda mawazo potofu! Yesu
ameonesha kwamba, ni chemchemi ya huruma kwa watu wote wanaomkimbilia. Mwanamke Msamaria
anaonja nguvu ya upendo inayomletea mabadiliko ya ndani, kiasi cha kukimbia na kwenda
kuwatangazia watu matendo makuu ya Mungu yaliyomwezesha kupata maji ya uzima wa milele,
maji ambayo alikuwa anayatafuta kwa udi na uvumba!
Mwanamke Msamaria anakwenda
Kijijini kwake, kule ambako watu wengi walikuwa wanamwangalia kwa "jicho la kengeza"
kutokana na maisha yake, lakini aliwatangazia kwamba, amekutana na Masiha aliyemwonesha
mwelekeo mpya wa maisha. Kila mara mwamini anapokutana na Yesu, maisha yake yanabadilika,
anasema Baba Mtakatifu, changamoto ya kukimbilia upendo wa Mungu, ili kugundua maana
ya maisha ya Kikristo yanayopata chimbuko lake kutoka katika Kisima cha Ubatizo.
Baba
Mtakatifu anawahamasisha waamini kuwashirikisha wengine ile furaha ya kukutana na
Yesu anayebadili mwelekeo wa maisha yao, kiasi cha kuwawezesha kuwamegea wengine ile
furaha inayobubujika kutoka katika undani wa maisha yao!
Baba Mtakatifu mara
baada ya Sala ya Malaika wa Bwana, amewakumbuka wagonjwa wa Kifua Kikuu, Jumuiya ya
Kimataifa inapoadhimisha Siku ya Kifua Kikuu, tarehe 24 Machi, 2014. Amezungumzia
pia Siku kuu ya Upatanisho, itakayoadhimishwa hapo tarehe 28 Machi 2014 kwa Makanisa
kuwa wazi ili kutoa fursa kwa waamini kujipatanisha na Mungu pamoja na jirani zao.