Kunako Mwaka 1993 Kanisa lilianzisha Siku ya Mashahidi Wamissionari Duniani, kama
sehemu ya mchakato wa Kumbu kumbu endelevu ya mauaji ya Askofu mkuu Oscar A. Romero
wa Jimbo kuu la San Salvador, yaliyotokea kunako tarehe 24 Machi 1980. Tangu wakati
huo, kila mwaka ifikapo tarehe 24 Machi, Kanisa lina sali na kufunga kwa ajili ya
kuwakumbuka na kuwaombea Wamissionari wote walioyamimina maisha yao kwa ajili ya kutangaza
Habari Njema ya Wokovu sehemu mbali mbali za dunia.
Kauli mbiu inayoongoza
maadhimisho ya Sku ya XXII kwa Mwaka huu ni “Ushuhuda”, kigezo msingi kwa kila mfuasi
wa Kristo kadiri ya maisha na utume wake ndani ya Kanisa. Waamini wanachangamotishwa
kuendele kuwa ni mashahidi amini wa Kristo hata katika nyakati hizi za utandawazi
na maendeleo ya sayansi na teknolojia. Washuhudie jeuri ya imani yao baada ya kukutana
na Kristo Mfufuka anayewapatia hamasa ya kusonga mbele kwa ari na moyo mkuu licha
ya madhulumu na nyanyaso wanazokabiliana nazo katika hija ya maisha yao hapa duniani.
Kamwe waamini hawapaswi kukata tamaa hata pale wanaposhindwa kueleweka wakati
wa mchakato wa Uinjilishaji Mpya. Kunako Mwaka 2013, Shirika la Habari za Kimissionari,
Fides linasema kwamba, kuna Mapadre 20, mtawa mmoja na waamini walei wawili waliouwawa
kutokana na imani yao kwa Kristo na Kanisa lake. Wamissionari hawa walioyamimina maisha
yao kwa ajili ya Injili wanapaswa kukumbukwa ili kukoleza ari na moyo kwa Wakristo
kutoka kimasomaso kutangaza Injili ya Kristo pasi na woga; kwa kusimama kidete kulinda
na kutetea haki msingi za binadamu, uhuru wa kuabudu, utu na heshima ya binadamu.
Mchango uliokusanywa katika mkesha wa Siku ya Mashahidi wamissionari Duniani,
itasaidia kugharimia miradi ya kimissionari nchini Tanzania hasa katika mikakati ya
majiundo makini kwa Majandokasisi nchini Tanzania.