Shemasi ni mhudumu wa Neno la Mungu, msaidizi mkuu katika huduma Altareni na katika
kumwilisha matendo ya huruma yanayotekelezwa na Mama Kanisa kwa ajili ya maskini na
wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii. Ushemasi ni kielelezo cha upendo wa Mungu,
unaomkirimia mwamini kuingia na kuishi katika huduma, kama alivyofanya Yesu mwenyewe
kwa kumwilisha upendo na huruma ya Mungu kwa binadamu.
Ni sehemu ya mahubiri
yaliyotolewa na Askofu msaidizi Paolo Selvadagi wa Jimbo kuu la Roma, wakati wa Ibada
ya Misa Takatifu kwa ajili ya kumpatia Daraja la Ushemasi wa mpito Frt. Marko Mapinduzi
Mwasatila Simbeye wa Shirika la Wamissionari wa Consolata, Ibada iliyofanyika kwenye
Parokia ya Msalaba Mtakatifu, Jimbo Kuu la Roma, Jumamosi, tarehe 22 Machi 2014.
Askofu
msaidizi Selvadagi anasema kuna furaha kubwa kwa Mama Kanisa kupata mhudumu kwa ajili
ya Kanisa na Ulimwengu katika ujumla wake. Hiki ni kielelezo cha upendo wa Mungu kwa
waja wake; upendo unaojionesha katika Maadhimisho ya Liturujia ya Kanisa, Mwenyezi
Mungu anapotukuzwa na mwanadamu kutakatifuzwa. Shemasi mpya atakuwa ni mhudumu wakati
wa maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu.
Shemasi amepewa dhamana ya kuwaonjesha
watu huruma na ukarimu wa Mungu kwa njia ya matendo ya huruma. Anatumwa kuwatangaza
na kushuhudia Neno la Mungu kwa njia ya maisha adili, manyofu na matakatifu. Anapaswa
kuwa makini kuwafafanulia watu yale yaliyojiri katika Neno la Mungu na kwamba, Shemasi
kimsingi ni mhudumu wa maskini mas wanyonge katika Jamii, watu ambao wanapata upendeleo
wa pekee katika maisha na utume wa Kanisa. Shemasi katika hija ya maisha yake, anapaswa
kumwilisha mashauri ya Kiinjili.
Shemasi Simbeye amepewa vifaa vya Ibada:
mavazi ya ushemasi, Neno la Mungu na Kalisi. Mara baada ya Misa Takatifu amewashukuru
wote waliomwezesha kufikia hatua hii na amewakumbuka wazazi na walezi wake ambao wako
Jimbo Katoliki la Mbeya, Tanzania. Ibada ya Misa takatifu imehudhuriwa na umati mkubwa
wa Familia ya Mungu kutoka Afrika Mashariki.