2014-03-24 09:23:32

Patriaki Ignatius Zakka wa Kwanza Iwas amefariki dunia!


Baba Mtakatifu Francisko amepokea kwa masikitiko makubwa habari za kifo cha Mheshimiwa sana Ignatius Zakka wa Kwanza Iwas, Patriaki wa Kanisa ya Kiorthodox la Syria na Antiokia aliyefariki dunia huko Ujerumani, tarehe 21 Machi 2014 alikokuwa anapata matibabu. Amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 80.

Wakristo wamempoteza Baba na kiongozi mashuhuri wa kiroho, aliyeonesha ujasiri wa pekee katika kuwaoongoza waamini wake nyakati za shida na magumu, tangu alipochaguliwa kunako Mwaka 1980. Katika maisha yake, ameshuhudia mateso na mahangaiko ya wananchi wanaoishi Mashariki ya Kati. Alikuwa ni kiongozi aliyejikita katika majadiliano ya kiekumene na amani, alipenda kuhakikisha kwamba, uhusiano kati ya Wakristo unaboreka maradufu. Ni kati ya Mababa waliohudhuria Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican, akajitahidi tangu wakati huo, kuimarisha uhusiano wa kiekumene na Kanisa Katoliki nchini Syria.

Baba Mtakatifu anamwombea pumziko la milele mbele ya Mwenyezi Mungu na kwamba, kifo chake, kiwe ni changamoto ya kuendelea kulihudumia Kanisa kwa ari na moyo mkuu sanjari na kukabiliana na changamoto zinazojitokeza katika maisha na utume wa Kanisa.







All the contents on this site are copyrighted ©.