Papa aunda Tume ya kusimamia ulinzi wa watoto wadogo dhidi ya nyanyaso za kijinsia
Baba Mtakatifu Francisko ameanzisha Tume ya Kipapa kwa ajili ya ulinzi kwa watoto
wadogo dhidi ya nyanyaso za kijinsia kama ilivyokuwa imekwisha tangazwa kunako tarehe
5 Desemba 2013. Tume hii inaundwa na Makleri pamoja na waamini walei, baadaye itaongezewa
nguvu na wajumbe kutoka sehemu mbali mbali za dunia. Lengo ni kuandaa katiba, mwongozo
na shughuli za tume hii.
Akizungumzia kuhusu tume hii, Padre Federico Lombardi,
msemaji mkuu wa Vatican anabainisha kwamba, Tume hii itakuwa ni msaada mkubwa kwa
Baba Mtakatifu Francisko katika utekelezaji wa utume wake kwa kuhakikisha kwamba,
watoto na vijana wanaishi katika mazingira yenye usalama, amani na utulivu kwa ajili
ya makuzi na majiundo yao kiroho na kimwili. Tume hii inaundwa na wanawake wanne,
ambao wamekuwa mstari wa mbele katika harakati za kutetea utu na heshima ya watoto
wadogo dhidi ya nyanyaso za kijinsia.
Tume ya Kipapa ni mwendelezo wa utekelezaji
wa mikakati iliyoanzishwa na watangulizi wake katika kulinda watoto na vijana dhidi
ya nyanyaso za kijinsia ambazo zilijitokeza katika miaka ya hivi karibuni na hivyo
kuchafua utume na maisha ya Kanisa. Huu pia ni utekelezaji wa ushauri uliotolewa na
viongozi wa Kanisa na wataalam katika masuala ya malezi na makuzi ya watoto.