2014-03-24 11:47:55

Hospitali ya Rufaa ya Nelson Mandela kwa ajili ya magonjwa ya watoto kuanza kazi 2017


Bara la Afrika linaendelea kumuenzi Mzee Nelson Mandela, aliyesimama kidete kulinda na kutetea: haki na amani; ukweli na uwazi; demokrasia na mafao ya wengi ndani na nje ya Bara la Afrika. Hivi karibuni, kumewekwa jiwe la msingi kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali ya Watoto, inayotarajiwa kuanza kufanya kazi ifikapo mwaka 2017. Hii inatarajiwa kuwa ni Hospitali kubwa ya rufaa kwa ajili ya magonjwa ya watoto kutoka katika nchi zilizoko Kusini mwa Afrika, itajengvwa mjini Johannesburg, Afrika ya Kusini.

Itakumbukwa kwamba, Barani Afrika kuna Hospitali kubwa za rufaa kwa watoto wagonjwa, huko Nairobi, Kenya na Cairo, Misri. Mchakato wa kuanzisha Hospitali ya rufaa kwa ajili ya magonjwa ya watoto anasema Sibongile Mkabile, mkurugenzi wa Hospitali hii ni kutaka kuokoa maisha ya watoto wadogo wanaoendelea kupoteza maisha yao kutokana na ukosefu wa huduma makini. Hospitali ya Kumbu kumbu ya Nelson Mandela, itakapokamilika itakuwa na vitanda 220.

Hii ni Hospitali ya binafsi, lakini inayolenga kutoa huduma hata kwa familia maskini, kwani kwa kawaida huduma za matibabu Afrika ya Kusini ni za ghali na mara nyingi wanaofaidika ni familia zenye uwezo mkubwa zaidi wa kiuchumi.







All the contents on this site are copyrighted ©.