2014-03-24 08:37:43

Hakuna maendeleo ya kweli pasi na amani!


Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe aliomwandikia Askofu mkuu Paolino Lukudu Loro wa Jimbo kuu la Juba, Sudan ya Kusini na kusomwa na Kardinali Peter Turkson, Rais wa Baraza la Kipapa la haki na amani, Jumapili iliyopita wakati wa ziara yake ya mshikamano na wananchi wa Sudan ya Kusini anakazia umuhimu wa kusitisha vita nchini humo ili kujielekeza katika majadiliano ya kina yanayolenga kudumisha misingi ya haki, amani, upendo na mshikamano wa kitaifa.

Baba Mtakatifu katika ujumbe huu ambao umeandikwa kwa niaba yake na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican anasema kwamba, hakuna maendeleo pasi na amani. Sudan ya Kusini ambayo ni taifa changa kabisa Barani Afrika lililojipatia uhuru wake kunako Mwaka 2013, limejikuta likitumbukia tena katika vita ya wenyewe kwa wenyewe, jambo ambalo linakwamisha mchakato wa maendeleo kwa wananchi wengi wa Sudan ya Kusini. Vita inaendelea kugharimu maisha ya watu wasiokuwa na hatia; inaleta utengano, umaskini, njaa, magonjwa na vifo.

Baba Mtakatifu anasema, watu waguswe kutokana na mahangaiko ya wananchi wa Sudan; wanaoendelea kutafuta hifadhi kwenye kambi za wakimbizi, watu ambao utu na heshima yao inadhalilishwa kana kwamba, hawana makwao! Baba Mtakatifu anaiomba Jumuiya ya Kimataifa kusaidia mchakato wa upatanisho, haki na amani nchini Sudan ya Kusini kwa kusimamisha vita ili kujikita zaidi katika majadiliano. Watu wapatie msaada wa hali na mali katika kipindi hiki kigumu cha maisha na historia yao na kwamba, mafao ya wengi yanapaswa kupewa kipaumbele cha kwanza kuliko kujikita katika ubinafsi, uchu na uroho wa mali na madaraka!

Baba Mtakatifu anasema, kuna haja ya kujenga na kudumisha utamaduni wa kukutana na kujadiliana, kwa kuthaminiana na kuheshimiana kama ndugu na wala si kama maadui, ili kwa pamoja kujenga mazingira ya amani na utulivu yanayojikita katika misingi ya maadili, kijamii na kiutu!

Baba Mtakatifu anasema, kipindi hiki cha Kwaresima iwe ni fursa ya kufanya toba na wongofu wa ndani, tayari kujitakasa, kwa njia ya sala, tafakari ya kina ya Neno la Mungu, kufunga na kujinyima kwa ajili ya kusaidia mchakato wa haki, amani na upatanisho.

Kardinali Turkson akiwa nchini Sudan ya Kusini ametabaruku Kanisa la Parokia ya Mtakatifu Yosefu, Jimbo kuu la Juba. Amekutana na kuzungumza na Baraza la Maaskofu Katoliki Sudan ya Kusini na viongozi wengine wa kidini pamoja na viongozi wa Serikali ya Sudan ya Kusini. Makundi yote haya yamekabidhiwa ujumbe kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko!







All the contents on this site are copyrighted ©.