Mpendwa msikilizaji wa Radio Vatican, tujumuike pamoja katika kipindi chetu cha Kanisa
la nyumbani. Tukiwa ndani ya kipindi cha Kwaresma, leo tunataka kutafakari juu ya
Fumbo la Msalaba wa Kristo.
Mama Kanisa
katika mafundisho yake, kwa mwanga wa Injili daima ametualika sote, kuyapatanisha
maisha yetu na Fumbo la Msalaba wa Kristo. Msingi wa fundisho hili ni mwito wa Bwana
mwenyewe anaposema “Mtu ye yote akitaka kunifuata, ni lazima ajikane mwenyewe, auchukue
Msalaba wake, anifuate” Mk. 8:34. Kipindi cha kwaresma tunatafakari safari nzima ya
Ukombozi ya Kristo, na tunataka kuona ni namna gani sisi, kila mmoja wetu kwa nafsi
yake ameuitikia mwito wa kuuchukua msalaba wa maisha na kumfuasa Kristo.
Kuuchukua
msalaba wa Kristo na kumfuata maana yake nini? Kuuchukua msalaba haimaanishi tu kuyaambata
maisha yetu ya mateso na matatizo ya kila siku. Njia ya msalaba ni safari ya nzima
ya Ukombozi ya Kristo. Safari hiyo ya ukombozi ni jumla ya mambo yote ambayo Bwana
Yesu aliyafanya, ili kumuunganisha Mwanadamu na Mungu. Yesu alifanya mengi ili kutukomboa,
hakuteseka tu (alifundisha, alihubiri, aliwalisha watu, aliwapa matumaini, alikemea
maovu, alisali, aliponya wagonjwa, na mwisho akahitimisha hayo yote kwa kujisadaka
yeye mwenyewe. Alifanya hayo yote ili kutuunganisha sisi wanadamu na Muumba wetu,
ambaye tulimwasi kwa dhambi zetu.
Hivyo, Msalaba ni jumla ya mambo yote ambayo
yanatuunganisha na Mungu. Msalaba ni ile kalisi ya wokovu inayotajwa na mzaburi katika
zaburi ya 116. Mwaliko wa Yesu kuuchukua msalaba, ni kuwa tayari kukipokea kikombe
hicho cha wokovu kila siku, na kuliitia jina la Bwana, yaani kumweka Mungu katika
maisha yetu ya kila siku, kuonja uwepo wake na kutegemea wema, msaada na huruma yake
daima.
Kuuchukua Msalaba na kumfuasa Yesu maana yake ni kuishi kama alivyotufundisha
Yesu mwalimu na kiongozi wetu. Ni kuwa pamoja naye daima. Kama twafurahi tufurahi
katika Bwana, kama twateseka, tuteseke pamoja naye, kama tukifa na tufe katika Bwana.
Kuuchukua msalaba wetu na kumfuasa, ni mwaliko wa kusali kama alivyosali yeye, kupenda
kama alivyopenda yeye, kufariji kama alivyofariji yeye, kuvumilia kama alivyovumilia
yeye, na mwisho wa yote tuwe sadaka kwa wokovu wa wengine kama alivyo yeye mwenyewe.
Ili kutekeleza vema wito na wajibu huo, tunahitaji imani thabiti.
Mpendwa msikilizaji,
kila mmoja katika maisha yake ya kila siku anacho kikombe chake cha wokovu, anao msalaba
wake. Kikombe changu cha wokovu na msalaba wangu ni tofauti kabisa na wa kwako. Katika
kikombe chako cha wokovu, kuna nyakati za heri zenye mambo mema, kuna nyakati za uchungu
na mateso, kuna nyakati za kukata tamaa, kuna nyakati za kujisikia mpweke kiroho na
kijamii nk. Kikombe hicho cha wokovu kinajidhihirisha katika nyakati zetu kihistoria
kadiri ya uradhi wa Mungu mwenyewe. Analotualika Yesu kufanya hapa, kwanza ni kutambua
kuwa tunabeba dhamana ya Ukombozi.
Kila mmoja katika kipindi hiki cha kwaresma,
analenga kujipatanisha na kujiambatanisha na Yesu, ili jinsi Yesu alivyo faraja kwa
wenye shida, sisi na tuwe hivyo; jinsi Yesu alivyo mwalimu wa ukweli kwa watu, na
sisi tuwe hivyo kwa wote wanaopotoshwa na yule mwangamizi wa ulimwengu huu! Jinsi
Yesu alivyokuwa huruma na msamaha kwa wakosefu, sisi nasi tuwasamehe na kuwahurumia
wakosefu!
Jinsi Yesu alivyo tumaini la waliojikatia tamaa, sisi nasi tuwafumbue
macho waliofunikwa na giza la udanganyifu wa ulimwengu huu. Kuuchukua msalaba ni mwito
wa kuwa karibu zaidi na Mungu na kuwa karibu zaidi na mwanadamu mwenzetu ili tusaidiane,
tuimarishane na tusindikizane katika safari yetu ya kuupanda mlima wa Bwana na kuketi
patakatifuni pake.
Katika Kanisa letu la nyumbani, yaani katika familia zetu
ambayo kweli ni shule ya fadhila mbalimbali, ni jukumu letu sote kama wanafamilia,
kusaidiana, kuinuana, kushikana mkono katika safari yetu ya kiroho, ili kila mmoja
aonje upendo na faraja katika familia. Ni katika familia mwanadamu anafundishwa kuwa
jirani na mwanadamu Mwenzake. Ni katika familia mwanadamu anafundishwa kuonja na kushiriki
upendo, furaha, huzuni na sikitiko la mwanadamu mwenzake. Hatuwezi kuwa wakombozi
kwa wenzetu endapo hatuonji shida na maumivu yao au hatuonji uwepo wao katika maisha
yetu. Ni katika familia tunajifunza kuvaa maisha ya mwanafamilia mwenzetu.
Ni
katika familia mwanadamu anafundishwa kuwa ubinafsi na kujipendelea ni dhambi. Tunaomba
na kusihi sana, humo katika familia, watu wafundishwe thamani ya Msalaba na hivyo
wawe tayari kuwasaidia wote wenye kulemewa na mizigo mizito ya maisha. Tuyapatanishe
maisha yetu na Fumbo la Msalaba wa Kristo, Msalaba ni njia ya kuupandia mlima wa
Bwana. Kutoka Studio za Radio Vatican, ni mimi Padre Pambo Martin Mkorwe OSB.