2014-03-22 10:17:50

Uchaguzi wa Jumuiya ya Ulaya, usaidie kujenga na kuimarisha mshikamano wa upendo na udugu


Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Jumuiya ya Ulaya, COMECE, linawaalika waamini na wananchi katika ujumla wao kuhakikisha kwamba, wanajikita katika kujenga na kuimarisha umoja na mshikamano, wakati wa uchaguzi mkuu wa Jumuiya ya Ulaya, unaotarajiwa kufanyika kati ya tarehe 22 hadi tarehe 25 Mei, 2014. Kardinali Reinhard Marx, Rais wa COMECE anabainisha kuhusu athari za myumbo wa uchumi kimataifa, lakini zisiwe ni kikwazo katika ujenzi wa utamaduni wa mshikamano wa upendo miongoni mwa Jumuiya ya Kimataifa.

Maaskofu katika mkutano wao, wanawataka wananchi wa Jumuiya ya Ulaya kuwa makini na viongozi watakaowachagua kuongoza kwa kipindi cha Miaka mitano. Vipaumbele na uchaguzi wao, uongozwe kwa namna ya pekee na Mafundisho Jamii ya Kanisa; utu na heshima ya binadamu, mafao ya wengi; haki na amani. Wananchi wa Bara la Ulaya wanapaswa kushiriki kwa wingi kabisa katika uchaguzi mkuu wa Jumuiya ya Ulaya kwani, tangu Mwaka 2008, Jumuiya ya Kimataifa ilipojikuta inakabiliwa na mtikisiko wa uchumi kimataifa, watu wengi wamekata tamaa na masuala ya kisiasa, kiasi kwamba, hawaoni tena sababu ya kushiriki kwenye chaguzi mbali mbali.

Nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya pamoja na wananchi katika ujumla wao, wahakikishe kwamba, wanaweza kando masilahi ya nchi husika kwa kujikita katika mafao ya wengi, ili kuwajengea watu matumaini yatakayowasaidia kukabiliana na changamoto mbali mbali zinazoendelea kujitokeza kwa wakati huu, kwa kujikita katika mshikamano wa upendo na udugu.

Baraza la Maaskofu wa COMECE linasema, kwamba, sera na mikakati ya maendeleo kichumi na kijamii haina budi kwanza kabisa kuzingatia utu na heshima ya binadamu, aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Maisha ni zawadi kutoka kwa Mungu inayopaswa kuheshimiwa, kulindwa na kuendelezwa tangu pale mtoto anapotungwa mimba tumboni mwa mama yake. Waamini na watu wote wenye mapenzi mema wasikubali kumezwa na utamaduni wa kifo.

Ikumbukwe kwamba, familia ina umuhimu wake katika maisha ya Kijamii na Kikanisa, kumbe, inapaswa kuheshimiwa na kusaidiwa kutekeleza dhamana na majukumu yake barabara. Jumuiya ya Ulaya inapaswa kuboresha sera na mikakati yake kuhusu wahamiaji na wageni wanaotafuta hifadhi ya maisha Barani Ulaya, kwa kuonesha mshikamano wa dhati na nchi wanachama wa Jumuiya ya Ulaya.

Uhuru wa kidini na umuhimu wa kuheshimu Jumapili kama siku ya mapumziko ni kati ya mambo ambayo yamegusiwa pia na Maaskofu katika ujumbe wao, unaohitimishwa kwa kutoa mwaliko kwa wananchi wote wa Umoja wa Ulaya kushiriki kikamilifu katika uchaguzi mkuu utakaofanyika kuanzia tarehe 22 hadi 25 Mei, 2014.







All the contents on this site are copyrighted ©.