2014-03-22 07:05:54

Mwanamke Msamaria anakutana na "Kyasaka"


Mwanamuziki Mbaraka Mwinshehe, aliimba: “Ugeni tabu ndugu zangu, unapofika nchi za mbali huwa mashaka. Hapo fikira za nyumbani hukujaa tele na majonzi kukujia mengi. Ugeni tabu mi’ nasema kweli si masihala wasafiri waelewa. Kwani unaweza tafuta kazi ukapata na pakulala ukawa huna. Ukabaki kuhangaika usiku kucha kwa sababu ya ugeni. Kweli nyumbani ni nyumbani nchi za kigeni hazina mazoea.” Wimbo huu unaonesha ukweli anaopambana nao msafiri au unapojikuta katika mazingira mazingira mageni ambayo wenyeji wake wanakushangaa na hawako tayari kukupokea.

Mtu ukiwa mgeni katika mazingira au pahala usipozaliwa yaani katika mazingira ya taifa jingine au hata kabila jingine, unaweza ukaitwa majina mengi sana hata majina ya kebehi, unawezwa ukaitwa mtu wa kuja; kyasaka, mnyamlenge, mpoma, mgeni, nk. Kama ni mgeni katika mazingira ya dini nyingine, hapo unaweza kuitwa kafiri, mromani, likristu, nk. Kwa vyovyote kuwa mgeni ni karaha sana hasa kama hutaki kujipokea na kujikubali kwamba wewe ni mgeni, mnyamlenge, mtu wa kuja, mpoma, kafiri, mkristu, mromani, nk. Unahitaji pia busara au diplomasia ya hali juu sana ili kuweza kuyatawala mazingira hayo, na hatimaye ukaweza kuyaathiri mazingira ambayo kwa mwanzoni yalikuona kwa jicho baya au hayakukupokea.

Leo tutakutana na mwanadiplomasia na mwanasaikolojia mkuu aliyepambana na mazingira mazito sana ya ugeni, lakini akafaulu kuyateka na kuyabadili. Injili inamwonesha Yesu kama mnyamlenge katika nchi ya Samaria. Alikuwa ametoka kusini Judea (Uyahudini) anaelekea nyumbani kwake kaskazini Galilea, hivi kwa vyovyote ilimbidi akatishe kana kupita katikati ya nchi ya Samaria. Hapo ndipo kilipompata kisanga cha kujisikia mgeni kwenye ardhi hiyo. Siyo tu yeye alijisikia mgeni bali alionwa hivi kama mtu wa kuja, mtu wa utamaduni tofauti na wasamaria tena na mwanamke. Watu wa makabila hayo mawili Wasamaria na kabila la Yesu (Wagalilaya) walikuwa hawaivani kabisa kiutamaduni. Zaidi tena Yesu alitazamwa kama mtu mwenye imani au dini tofauti na ile ya wasamaria yaani walitofautiana kiitikadi.

Katika mazingira kama hayo, utaona jinsi Yesu alivyo gwiji wa saikolojia anavyoweza kukabiliana na mazingira magumu, anavyosikiliza, anavyohoji mambo, na kutoa rai zake, hadi anafikia hali ya kuanzisha mazungumzo (dayalogu) mazuri yanayolainisha na kugeuza moyo mwa mpinzani wake. Hali ambayo ni kama kuanzisha “uzao upya”. Mnaweza kirahisi kulinganisha na kutofautisha dayalogu au mazungumzo yalivyokuwa kati ya Ibilisi na Yesu kule jangwani (Dominika ya kwanza kwaresima) na mazungumzo haya ya kati ya mwanamke huyu msamaria na Yesu kwenye kisima (chemchemi) ya maji.

Mapato ya mazungumzo ya hapa kisimani, yanatokana na uhuru aliokuwa nao Yesu, hadi kufanikisha kuathiri mazingira yaliyokuwa magumu sana tena yaliyokuwa dhidi yake. Hali hii inaonesha wazi kwamba Yesu ni mwalimu wa utu kwa wote, mdiplomasia na msaikolojia mkuu. Ni mwalimu kwa sababu anao uweza wa kuvuka vizuizi vinavyopinga majadiliano. Mipaka au vizuizi vile vinavyomtenga mwanaume na mwanamke, mipaka kati ya watu wa eneo moja hadi jingine; kati ya watu wa makabila tofauti. Ukitaka kujifunza utu wema, saikolojia na diplomasia ya kweli na kuweza kuanzisha na kuendesha dayalogu ya aina yoyote hata ile ya kisiasa, basi jaribu kufuatana na Yesu katika Injili ya leo.

Mchokozi rasmi wa majadiliano hayo ni Yesu anayeomba: “Nipe maji ninywe”. Majibu ya mwanamke yule ndiyo yanayoonesha kuwa Yesu ni mtu wa kuja katika kabila jingine: “Imekuwaje wewe mgeni kuniomba mimi maji ya kunywa, nami ni mwanamke Msamaria?” Jibu kama hili linatosha kabisa kukukatisha tamaa na kuendelea kuomba maji. Mwanamke huyu anamwonesha Yesu kuwa hawana mahusiano yoyote kikabila wala kijinsia. Kwani kati ya myahudi rabi na mwanamke haikuwezekana wala haikuruhusiwa kabisa kuzungumzana. Kumbe Yesu akiwa kama mwalimu wa uzima kwa sababu Yeye ni chemchemu unapotoka uzima. Anaanzisha mazungumzo na kukutanisha watu ambao wamekata kabisa mawasiliano, wala kupeana mikono. Yesu anaanzisha mazungumzo na mahusiano kwa kuanza na ufukara wake: “Nina kiu” (Nipe maji ninywe). Tujifunze kutoa kama anavyotoa Yesu. Kama mtu fukara anayepokea, kutoa kwa fukara, kwa watu wa kuja (wageni) na siyo kwa ukuu kama ule wa mtu tajiri, bali kwa unyenyekevu wa watu fukara. Anayejua kuwa anaweza kupokea zaidi endapo anajali utu. Yesu anafaulu kumzaa mwanamke mpya. Anapozungumza na wanawake anawagusa moyo moja kwa moja. Anajua lugha zao, lugha ya kutamani lugha ya vionjo, lugha ya kutafuta hoja nzito za kuishi.

Kuhusu kupambana na ugeni wa mazingira ya imani (dini) tofauti, ni pale Yesu anapokubaliana na kauli ya mwanamke kwamba anaishi na mshikaji wa sita baada ya kuachika na washikaji wengine watano “Hapo umesema kweli.” Hapo mwanamke anaanza kuthibitisha kutofautiana kwao katika imani: “Baba zetu waliabudu katika mlima huu, nanyi husema ya kwamba huko Yerusalemu ni mahali patupasapo kuabudia.” Tamko hili la mwanamke linaonesha wazi kwamba wao ndiyo wanaofuata mapokea ya mababu ya kuabudu katika mlima, wakati dini ya Yesu ni maagizo ya watu wa siku hizi waliojijengea tu hekalu Yerusalemu na kuabudu. Yesu anachukua mwanya huu wa kutofautiana kiitikadi za imani na kumfundisha mwanamke yule akisema: “Ninyi mnaabudu msichokijua; sisi tunaabudu tukijuacho; kwa kuwa wokovu watoka kwa Wayahudi. Lakini saa inakuja, nayo sasa ipo ambayo waabuduo halisi watamwabudu Baba katika roho na kweli...” Hapa Yesu anaenda zaidi ya pale anapofahamu mwanamke na kumwongezea uhondo zaidi wa kuabudu, yaani kuabudu Baba katika roho na kweli.
Ndipo sasa unapomwona Yesu anaibuka na namna mpya ya saikolojia, anaweza hata kupendekeza jambo linalohusu maisha binafsi ya mtu anapomwambia mwanamke: “Nenda kamwite mumeo, uje naye hapa.” Hapa ndipo mwanamke akajibu “Sina mume” kwa kweli angetakiwa aseme tu kwamba “Ninaye mshikaji.” Mwanamke huyu ni mithili ya wayahudi waliokuwa wametangaanawakilisha wale wanaoabudu miungu, sanamu, ni sawa na malaya. Mwanamke huyu ni mimi!

Yesu anasema: “Umesema vema, ‘Sina mume’; kwa maana umekuwa na waume watano naye uliye naye sasa siye mume wako; hapo umesema kweli.” Yesu hamhukumu yule mama msamaria tena hamdhalilishi, bali anasisitiza karibu mara mbili kwa kusema “Umesema kweli kabisa”. Yesu alishamtambua mwanamke huyo ni wa aina gani kutoka mwanzo alipofika kuketi pale kisimani mchana. Wanawake wa kawaida wanachota maji asubuhi sana au jioni, kwa hiyo anayeenda kuchota maji mchana tena peke yake anaweza kujulikana ni mwanamke wa aina gani na anatafuta nini. Kwa tamko hilo “Umesema kweli kabisa” Yesu hana nia ya kuharibu mahusiano waliyo nayo, bali anataka kumweka sawa mwanamke huyo kwamba hana budi kujiweka sawa kabla ya kujidhatiti kuyawania hayo maji ya uzima anayoyatamani. Aidha siyo Yesu anayetakiwa kuyapanga maisha ya mbele ya huyo mwanamke – bali ni kama vile angemwambia “Kazi kwako!” Upendo ni mlango wa Mungu na ni Mungu aliye ndani yetu. Ni Mungu anayetujali sana, ni Mungu mwenye utu wa hali ya juu sana, hiyo ndiyo sura nzuri ya Mungu.

Mwanamke alisema kuwa “Kisima kile ni kirefu kimezama sana.” Kiasi Yesu asingeweza kufanikiwa kuchota maji kwa vile hakuwa na kata (nyenzo) ya kuchotea. Endapo kisima hicho ni wewe na mimi, hapa unaona dhahiri kwamba ipo njia moja tu ya kuchota maji ya kisima hicho kilichozama sana cha kila mmoja wetu, nayo siyo kwa njia ya kugombeza, kukashifu, kukosoa, bali kwa njia ya kumfanya mmoja aonje utamu zaidi wa maisha, wa uzuri wa mali au kisima alicho nacho. Angalia Yesu anavyomtamanisha mwanamke huyu hadi anachoka mwenyewe anapomwambia: “Mimi nitakupa maji ambayo yanakuwa chemchemu”. Maji ni uzima, maisha, nguvu ya maisha, ambayo ninaipokea ninapojiunganisha na chemchemi isiyokauka ya maisha ambayo ni Mungu. Yesu anampa Mama Msamaria fursa ya kujiunganisha au kujisogezasogeza karibu na chemchemi yake ili baadaye yeye mwenyewe awe chemchemu.

Hiyo ni picha nzuri sana, picha ya maji yanayotembea, inayobubujika, mto wa uzima ni zaidi ya ule unaozima kiu yako tu, bali ni mto ule unaozima hata kiu ya wengine. Chemchemu haimilikiwi bali inajieneza, inazaa. Kwa ahadi kama hiyo ya Yesu, yule mwanamke msamaria anaelewa kwamba hataweza kutuliza kiu yake kwa kunywa na kusaza, bali kwa kutuliza kiu ya wengine. Kwamba ataangazwa tu kwa kuangaza wengine, atapata furaha kwa kutoa furaha kwa wengine. Kuwa chemchemi: ni mradi mzuri wa maisha, ni chemchemi ya matumaini, ya kupokea, ya upendo. Baada ya kuuelewa ukweli huu juu ya chemchemi, hapo ndipo sasa, mwanamke yule anautelekeza mtungi wa maji pale kama vile ungekuwa kitenge kilichochakaa, anaacha maisha ya zamani, anakimbia kwenda mjini na kumsimamisha kila anayepita barabarani. “Jamani! kuna mtu kisimani huko, anayekuwezesha uzaliwe na kuzaliwa tena upya. Usipozaliwa hujaumbika. Njoni mumtazame mtu aliyeniambia mambo yote niliyoyatenda.” Anakuambia mambo yaliyoko katika moyo wako na kuiibusha chemchemi.

Mwanamke huyu anahaha huku na huku, anakimbiakimbia, anaita, anashuhudia, anafanya unabii, anawachemsha watu wote, na hadi anazungukwa na jumuia mpya ya kwanza ya wafuasi wageni. “Basi wakatoka mjini, wakamwendea.” (Yohane 4:30). Na katika mji ule Wasamaria wengi walimwamini kwa sababu ya maneno ya yule mwanamke aliyeshuhudia kwamba, “aliniambia mambo yote niliyoyatenda.” Basi wale Wasamaria walipomwendea, walimsihi akae kwao; Watu wengi zaidi wakaamini…” (Yoh 4:39-40). Kuna mmoja, Yesu, anayejua na kusema yote juu yako. Yeye anajua kilicho ndani ya mioyo yetu: Jema lina nguvu zaidi kuliko bovu au baya, kuna jema lililo kongwe zaidi kuliko ubaya, kuna jema linawezekana kuwa muhimu zaidi kuliko ubaya wa sasa. Kuna ziwa la nuru na uwepo wake ndani mwetu ndiyo unaokuwa chemchemu.

Kwa hiyo nitaenda wapi ili kuwambudu Mungu? Siyo mlimani, siyo hekaluni au Kanisani!. Bali katika mimi: ni mimi ndiye ule mlima wa Mungu, mimi ni Kanisa. Naye ni chemchemi ya chemchemi zangu. Hata sisi, kama yule mama msamaria, anayeenda kisimani kuchota maji na anarudi ametajirika, kama tukimpokea Mungu ndani yetu anayetufanye tuzaliwe upya, anayebomoa kila kizuizi, mpaka, hapo tutaona kububujika kati ya mikono yetu wimbo wa chemchemu. Pahala popote pageni utakapokuwa, hali yoyote ile chukivu, mtazamo wowote ule mbaya wa maisha utaweza kuubadili kwa mazungumzo ya upendo, bora tu ukijifunza toka kwa Yesu.
Padre Alcuin Nyirenda, OSB.








All the contents on this site are copyrighted ©.