Rais George Abela wa Malta akutana na kuzungumza na Papa Francisko mjini Vatican
Baba Mtakatifu Francisko, Ijumaa tarehe 21 Machi amekutana na kuzungumza na Rais George
Abela, Rais wa Malta ambaye baadaye alikutana na Kardinali Pietro Parolin, Katibu
mkuu wa Vatican aliyekuwa ameambatana na Askofu mkuu Dominique Mamberti, Katibu mkuu
wa mambo ya nchi za nje za ushirikiano wa kimataifa mjini Vatican.
Mazungumzo
kati ya Baba Mtakatifu Francisko na mgeni wake yamefanyika katika hali ya utulivu
kabisa kwa kupembua Ukristo katika historia, utamaduni na maisha ya wananchi wa Malta
sanjari na uhusiano wa karibu kati ya Nchi hizi mbili, kama inavyojidhihirisha katika
hija za kichungaji zilizofanywa na Mwenyeheri Yohane Paulo II na Baba Mtakatifu mstaafu
Benedikto XVI.
Kwa namna ya pekee mazungumzo ya viongozi hawa wawili yamejikita
katika uhusiano kati ya Kanisa na Serikali ya Malta na mchango wa Kanisa katika sekta
ya elimu na huduma za kijamii; mikataba iliyotiwa sahihi kati ya pande hizi kwa ajili
ya ushirikiano na mafao ya wengi. Wamejadili mchango wa Malta katika Jumuiya ya Ulaya
na Ukanda wa Mediterania, bila kusahau tatizo la wakimbizi linaloongezeka mwaka hadi
mwaka. Wameangalia mchango wa Serikali na Kanisa katika kuwahudumia wahamiaji na watu
wasiokuwa na makazi maalum.