2014-03-21 07:39:24

Jumuiya ya Kimataifa inahitaji mikakati ya kilimo makini na endelevu


Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Bwana Ban Ki-Moon pamoja na Bwana Josè Graziano da Silva, Mkurugenzi mkuu wa Shirika la Kilimo na Chakula la Umoja wa Mataifa, FAO, wanaitaka Jumuiya ya Kimataifa kuibua sera na mikakati bora ya kilimo kama sehemu ya kushiriki kikamilifu katika Maadhimisho ya Mwaka wa Familia ya Wakulima Kimataifa. RealAudioMP3

Ni wajibu wa Serikali kusaidia mikakati ya wakulima wadogo wadogo kuweza kutekeleza wajibu wao kikamilifu. Serikali ziwajengee uwezo familia za wakulima hasa vijana na wanawake, kwa kuibua sera na mikakati itakayosaidia kukuza na kudumisha maendeleo ya sekta ya kilimo vijijini.

Mchakato huu hauna budi kwenda sanjari na maboresho ya miundo mbinu ya barabara, ili kupunguza kiwango cha uharibifu wa mazao unaofanyika tangu mazao yanapovunwa mashambani hadi pale yanapomfikia mlaji. Benki na vyama vya kutoa mikopo viwasaidie wakulima wadogo wadogo kupata mikopo ili kuinua kiwango cha uzalishaji.

Bwana Graziano da Silva anasema kwamba, wakulima wadogo wadogo wakiwezeshwa katika uzalishaji, Jumuiya ya Kimataifa inaweza kuwa na uhakika wa usalama wa chakula kwa siku za usoni. Utafiti uliofanywa katika nchi 93 unaonesha kwamba, asilimia 90% ya mashamba yanamilikiwa na familia, ambazo pia ni wamiliki wa ardhi. Asilimia 63% ya mashamba Barani Ulaya ndiyo yanayomilikiwa na familia.

FAO inasema kumezuka wimbi la kuwaponya wakulima vijijini ardhi waliyokuwa wanaimiliki kwa kisingizio cha kutaka kuwekeza katika kilimo cha kisasa, hali ambayo inaweza kusababisha kutoweka kwa amani na utulivu. Sheria na kanuni za utawala bora na kanuni za uwajibikaji makini katika uwekezaji kwenye sekta ya kilimo zinapaswa kuzingatiwa. Wawekezaji wataendelea kukwapua maeneo makubwa ya ardhi kwa ajili ya kuendeleza kilimo cha kisasa, kumbe jambo la msingi inasema FAO ni kuhakikisha kwamba, sheria na kanuni zinazingatiwa kwa ajili ya mafao ya wengi.








All the contents on this site are copyrighted ©.