Shukrani huainisha sala ya Kanisa ambalo kwa kuadhimisha Ekaristi Takatifu hujifunua
lilivyo na huwa kamilifu zaidi. Kwa kweli, katika kazi ya wokovu, Kristo huvifanya
viumbe huru kutoka katika dhambi na mauti ili kuvitakasa upya na kuvifanya vimrudie
Mungu Baba kwa ajili ya utukufu wake. Shukrani ya viungo vya Mwili hushiriki shukrani
za Kichwa chao.
Mtakatifu Paulo anawahimiza Wakristo kushukuru kwa kila jambo
kwani hayo ni mapenzi ya Mungu kwao kwa njia ya Yesu Kristo. Anawataka waamini kudumu
sana katika kuomba, wakikesha katika kuomba huku wakishukuru.
Baba Mtakatifu
Francisko wakati huu anapohitimisha Mwaka mmoja tangu alipochaguliwa kuliongoza Kanisa
Katoliki, anawaalika watumiaji wa mitandao ya kijamii kujifunza kumshukuru Mungu pamoja
na jirani. Hii ni dhana ambayo wazazi na walezi wanapenda kuwafundisha watoto wadogo,
lakini watu wazima wenyewe wanasahau kushukuru!