2014-03-20 09:37:13

Hali halisi ya Tanzania!


Tovuti ya Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican inaendelea kukumegea ujumbe wa Kwaresima kwa Mwaka 2014 kutoka Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, unaoongozwa na kauli mbiu "Ukweli utawaweka huru". Tumekwisha kukumegea kuhusu utangulizi, wongofu na ukweli unaowaweka huru waamini, wajibu wa kuuishi, kuulinda na kuusimamia ukweli kishuhuda. Leo tunakuletea sehemu ya tatu: hali halisi ya Taifa la Tanzania.Ndani ya viunga vya Radio Vatican kukujuza zaidi ni Padre Pambo Martin Mkorwe, OSB. RealAudioMP3


Taifa lenye umri wa miaka 50 ya uhuru ni taifa lililokwishavuka uchanga. Ni taifa kijana lililo katika umri wa kujenga juu ya misingi iliyowekwa kwa manufaa ya wote. Ni taifa linalojitegemea. Bila msingi huo, mengine yote, hata kama yanaonekana yanang’aa yatakuwa yanasaliti mustakabali wa kweli wa taifa letu.

Tusijidanganye. Bila msingi wa kujitegemea na kutafuta manufaa ya wote (common good) taifa hili litaanguka. Kama halianguki leo, kesho ni lazima litaanguka. Tunajiuliza, uko wapi ujasiri wa Taifa letu? Imepotelea wapi fahari ya kujitawala, si kisiasa tu, bali kiuchumi, kifikira na kijamii? Imepotelea wapi ile mbegu ya uzalendo iliyopandwa na waasisi wa taifa letu? Imeishia wapi heshima ya kuthamini utu, kuheshimu imani ya asiyeamini kile nisichokiamini na kutafuta ufumbuzi halisi wa matatizo yanayotukabili?


Tumepoteza dira ya kujitegemea kimaamuzi na kimkakati. Tumefikia mahali pa kuamini kwamba maendeleo yataletwa kwa kaulimbiu zinazobadilika badilika kila siku. Katika mazingira ya sasa, watu wachache, kwa sababu binafsi na kwa manufaa binafsi wanapotosha ukweli na kutafuta njia za kulinda maslahi yao kwa kutumia mifumo isiyokubalika, lakini inayosimikwa na kuhalalishwa ili kulinda maslahi binafsi. Hali hii inajidhihirisha kupitia matumizi mabaya ya madaraka, mikataba mibovu, kupindisha sheria, kufumbia macho uhalifu, nk.

Uhuru wa kweli haujengeki katika misingi dhaifu ya ubinafsi na haulengi kumfanya mtu yeyote yule awe juu ya sheria za haki na taratibu za uadilifu. Na kimsingi, hakuna maendeleo ya kweli kama watu hawaheshimu haki ya msingi ya kuujua ukweli na kuishi kadiri ya ukweli huo.

Katika mazingira kama haya Kanisa haliwezi kukaa pembeni na kutazama tu kwa sababu nalo lina wajibu wa kuijenga jamii. Kanisa lina wajibu wa kuangalia, kuboresha na kuikosoa mienendo ya kijamii na kisiasa inayohatarisha ustawi wa jamii nzima na hivyo kuathiri kazi ya Kristo ya kumkomboa mwanadamu na kuusimika Ufalme wa Mungu; ufalme unaojidhihirisha katika kutamalaki kwa ukweli, haki na amani. Kanisa litaendelea kusisitiza ukweli huu kwamba; “Ili kuunda maisha ya kisiasa yaliyo kweli ya kibinadamu, hakuna lililo bora zaidi kuliko kustawisha ndani ya watu hisia za haki, upendo na huduma kwa manufaa ya wote”. Hapa tungependa kuelezea mambo machache yanayoivuruga nchi yetu.

Usikose kujiunga nasi tena, kwa ufafanuzi zaidi wa mambo yanayoivuruga Tanzania katika mchakato wa kulinda, haki, amani, upendo, mshikamano na umoja wa kitaifa.










All the contents on this site are copyrighted ©.