2014-03-19 08:48:59

Miaka 50 iliyopita, Wacomboni walifungishwa vilago kutoka Sudan ya Kusini


Shirika la Wamissionari wa Comboni, Mwaka 2014 linafanya kumbu kumbu ya tukio la kihistoria, miaka hamsini iliyopita walipolazimishwa kufunga vilago na kuondoka mara moja kutoka Sudan ya Kusini. Hiki kilikuwa ni kipindi kigumu sana katika historia na maisha ya Shirika la Comboni Barani Afrika, lakini uvumilivu, subira na matumaini, yameliwezesha Kanisa Barani Afrika kuvuma matunda ya maisha na utume wa Kanisa linaloendelea kushamiri kwa kasi kubwa Barani Afrika.

Hivi ndivyo wanavyokumbuka Wamissionari wa Comboni, pale Serikali ya Sudan ilipoamua kunako Mwaka 1964 kuwafukuza wageni wote kutoka Kusini mwa Sudan, wakiwemo Wamissionari licha ya kwamba, wao walikuwa wanajihusisha katika mchakato wa Uinjilishaji wa Kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Wakuu wa Shirika la Wacomboni wanakumbuka hatua mbali mbali zilizochukuliwa na Shirika katika mipango yake ya kati na mirefu kwa ajili ya ustawi wa Kanisa Barani Afrika.

Tamko ya kuwafukuza Wamissionari wageni kutoka Sudan ya Kusini, lilitiwa mkwaju kunako mwaka 1964, hapo Wamissionari 300 wakafungishwa vilago kwa lazima na kuondoka Kusini mwa Sudan kwa kosa la kuingilia mambo ya ndani ya Sudan. Taarifa zinaonesha kwamba, katika kipindi cha siku kumi tu, Parokia 58 zikawa tupu! Sudan ya Kusini ikajikuta ikiwa imebaki na Askofu mmoja na Mapadre 28 tu. Huu ulikuwa ni ukurasa wa giza, mateso na mahangaiko kwa Wamissionari, lakini zaidi kwa Waamini na wanachi wa Sudan ya Kusini.

Wakuu wa Shirika la Wacomboni wanasema, katika machungu na mahangaiko ya Wamissionari wa nyakati zile, Mwenyezi Mungu ameonesha upendeleo wa pekee kwa watu wake, leo hii licha ya machafuko ya kisiasa Kusini mwa Sudan, Kanisa limeendelea kustawi na kushamiri kama mtende wa Lebanon. Kanisa Katoliki limesimama na kuimarika kwa kuwa na uongozi makini, kuanzia kwa Maaskofu, Mapadre na Watawa pamoja na Waamini ambao kwa pamoja wanajenga na kuimarisha Familia ya Mungu Kusini mwa Sudan.

Wamissionari wa Comboni wanaendelea kuombea amani, utulivu na mshikamano wa kitaifa, ili watu waendelee kuchakarika katika mchakato wa kujiletea maendeleo yao: kiroho na kimwili.







All the contents on this site are copyrighted ©.