2014-03-18 10:55:03

Wasaidieni wanawake kuona sura na mfano wa Mungu hata katika watoto ambao bado hawajazaliwa


Kanisa pamoja na watu wenye mapenzi mema wana dhamana ya kuhakikisha kwamba, wanawasaidia wanawake kusimama kidete kulinda na kutetea Injili ya Uhai, inayowawezesha kuiona ile sura na mfano wa Mungu hata miongoni mwa watoto ambao wako bado tumboni mwa mama zao. Ni changamoto ya kukataa katu katu kukumbatia utamaduni wa kifo, bali wanawake wawe mstari wa mbele kutangaza Injili ya Uhai kwa njia ya ushuhuda wa maisha yao ya kila siku.

Hii ndiyo changamoto inayotolewa na Askofu mkuu Jean Laffitte, Katibu mkuu wa Baraza la Kipapa la Familia, anayetarajiwa kushiriki katika Kongamano litakaloshirikisha vyama vya kitume na kiraia vinavyosimama kutetea Injili ya Uhai. Ni Kongamano hili litafanyika tarehe 22 Machi, 2014 kwenye Taasisi ya Kipapa ya Regina Apostolorum, iliyoko mjini Roma na limeandaliwa na Chama cha kutetea maisha pamoja na Bikira Maria.

Kanisa daima limetambua sura na mfano wa Mungu, changamoto ya kuendelea kusimama kidete kulinda na kutetea Injili ya Uhai. Kongamano hili ni sehemu ya maandalizi ya Maadhimisho ya Siku kuu ya Bikira Maria kupashwa habari kuwa atakuwa ni Mama wa Mungu, inayoadhimishwa kila Mwaka ifikapo tarehe 25 Machi. Hapa Kanisa linatafakari kuhusu Fumbo la Umwilisho, Neno wa Mungu alipotwaa mwili kwa njia ya Roho Mtakatifu na kukaa kwake Bikira Maria. Yesu mwenyewe katika maisha na utume wake, alitoa kipaumbele cha pekee kwa watoto wadogo, maskini na wagonjwa.

Mkristo anaalikwa kwa namna ya pekee kulitafakari Fumbo la Umwilisho kwa kumwangalia mwanadamu anayepewa upendeleo wa pekee mbele ya Mwenyezi Mungu pamoja na kukombolewa na Yesu Kristo kwa njia ya Msalaba. Askofu mkuu Jean Laffitte anasema, kuna uchungu mkubwa kwa mama anapompoteza mtoto wake. Kwa wanawake wanaotoa mimba, madhara yake ni makubwa katika maisha yao.

Haiwezekani sheria kuhalilisha vifo vya watoto wachanga kwa njia ya utoaji mimba, kwani kufanya hivi ni kwenda kinyume cha haki msingi za binadamu. Kuna haja kwa Waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kujenga na kuendeleza utamaduni wa Injili ya Uhai kwa kuwasaidia wanawake kutambua sura na mfano wa Mungu unaojionesha katika maisha ya watoto wao, hata kabla ya kuzaliwa







All the contents on this site are copyrighted ©.