Shirika la Misaada la Kanisa Katoliki Ureno, kuanzia tarehe 17 hadi tarehe 23 Machi
2014 linaadhimisha Juma la Kupambana na Baa la Njaa Kitaifa linaloongozwa na kauli
mbiu "Mshikamano wa upendo dhidi ya baa la njaa". Caritas Ureno inatumia kipindi hiki
kwa ajili ya kuhamasisha mshikamano wa upendo na udugu katika mchakato wa kupambana
na baa la njaa duniani.
Kati ya tarehe 20 hadi tarehe 23 Machi 2014, Caritas
itakusanya mchango kutoka kwa waamini na watu wenye mapenzi mema kwa ajili ya kugharimia
miradi mbali mbali inayoendeshwa na Kanisa Katoliki nchini Ureno. Waamini na wananchi
wote kwa ujumla, wanachangamotishwa kuhakikisha kwamba, wanashiriki kikamilifu katika
ujenzi wa jamii inayosimikwa katika haki, upendo na mshikamano wa kidugu. Kila mwananchi
akitekeleza dhamana na wajibu wake ndani ya Jamii, kuna uwezekano mkubwa wa kupata
mafao ya wengi.
Caritas Ureno inaungana na Shirikisho la Mashirika ya Misaada
ya Kanisa Katoliki Kimataifa, Caritas Internationalis katika kampeni dhidi ya baa
la njaa duniani ifikapo mwaka 2025. Hii ni Kampeni inayoongozwa na kauli mbiu "Familia
moja ya binadamu, chakula kwa wote" iliyozinduliwa Desemba 2013 kwa kumshirikisha
Baba Mtakatifu Francisko aliyetuma ujumbe wake kwa njia ya Video.