Jumuiya ya Kimataifa ikijizatiti, baa la njaa litapewa kisogo!
Bwana Kanayo Nwanze, Rais wa Mfuko wa Maendeleo ya Kilimo wa Umoja wa Mataifa, IFAD
katika mahojiano maalum na Radio Vatican anabainisha kwamba, Baba Mtakatifu Francisko
ni kiongozi ambaye anaguswa na baa la njaa duniani, jambo ambalo linajionesha katika
historia na maisha yake adili na manyofu. Ni kiongozi anayeendelea kuichangamotisha
Jumuiya ya Kimataifa kuleta mabadiliko katika maisha ya watu, kwa kuguswa na mateso
ya watu wanaoteseka kwa baa la njaa duniani.
Bwana Nwanze anasema, asilimia
30% ya chakula kinatupwa sawa na kutupa mabillioni ya fedha ambayo ingeweza kutumika
kuganga baa la njaa duniani. Takwimu zinaonesha kwamba, asilimia 20 hadi 40% ya chakula
kinachozalishwa inapotea njiani kabla hata ya kumfikia mlaji. Hapa kunaonesha jinsi
ambavyo chakula kinavyopotea na kutupwa na wakati huo huo, Jumuiya ya Kimataifa inasema
kwamba, kuna haja ya kujifunga kibwebwe ili kuongeza uzalishaji wa chakula kwa watu
billioni 9 ifikapo mwaka 2050.
Chakula kinachozalishwa duniani kwa wakati huu
kina uwezo wa kutosheleza mahitaji ya watu billioni 7.1. Jambo linalokwamisha upatikanaji
wa chakula kwa watu wengi zaidi ni ubovu wa miundo mbinu ya barabara hasa vijijini
na katika nchi zile ambazo zimeathirika vibaya kutokana na mabadiliko ya tabianchi.
Baba
Mtakatifu Francisko anaendelea kutoa changamoto kubwa kwa Jumuiya ya Kimataifa kushikamana
kama binadamu na kwamba, ni jambo lisilokubalika kwamba, watu zaidi ya billioni 1
waendelee kuteseka kutokana na utapiamlo na baa la njaa. Mashirika ya Misaada ya Umoja
wa Kimataifa yanadhamana na wajibu wa kuwapatia wananchi furaha sanjari na kuwajengea
uwezo ili waweze kupambana na baa la njaa, umaskini na maradhi.
Wakulima wadogo
wadogo wajengewe uwezo katika uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara; ili kuwa
na uhakika wa usalama wa chakula na pato kwa ajili ya kuboresha hali ya maisha ya
familia husika.